NA HAJI NASSOR, PEMBA
NGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Mwinyi, amewaahidi wakulima wa zao karafuu kisiwani hapa kwamba hakuna atakaepunjwa haki yake kama atachaguliwa kuwa Rais.
Alisema haridhishwi kuona watendaji wanaolipwa na serikali kuwaibia kwa makusidi wakulima wakati wanapokwenda kuuza karafuu zao.
Akizungumza na wakulima wa zao hilo,chumvi na viungo katika hoteli ya Wesha nje kidogo ya mji wa Chake- Chake, alisema hilo atalisimamia kwa dhati.
Alisema alichukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo, ili kuwatumikia wananchi wote wakiwemo wakulima.
Aidha, aliwaahidi wakulima wa karafuu kuwapatia mikopo ili kuimarisha kilimo hicho.
Dk. Mwinyi pia aliahidi kuwapatia mitaji wakulima wa chumvi na bidhaa za viungo.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Mabodi, alisema Dk. Mwinyi ni mchapakazi hodori na ndio sababu CCM ikamchagua kugombea nafasi hiyo.
Awali akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake wa karafuu, Sharif Maalim, alisema wakati umefika kwa wakulima kushajiishwa ili waweza kuzalisha miche kwa wingi kwa kutumia vilatu vyao.
Alisema serikali ijayo lazima iangalie upya fedha zinazoelekezwa kwa kikosi kazi cha kushughulikia zao la karafuu, badala yake fedha hizo zihamishiwe kwa wakulima.
“Wakulima wameamua kuuza karafuu zao ZSCT baada ya serikali kuongeza bei lakini kuna tatizo la kupunjwa tunapokwenda kuu kutokana na matumizi ya mezani zilizopitwa na wakati,” alisema.