Afungua ‘Terminal III’ AAKIA

Asema liongeza kasi ukuaji uchumi

NA LAILA KEIS

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa kukamilika kwa jengo la tatu la abiria kwenye uwanjwa wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kutaongeza mapato na kasi ya ukuaji wa uchumi.

Alieleza hayo jana alipokuwa akihutubia wananchi na viongozi mbali mbali baada ya kulifungua jengo hilo (terminal III), Kisauni, wilaya ya Magharibi ‘B’, Unguja.

Alisema, uimara na ukubwa wa miundombinu katika uwanja huo kutochochea wingi wa mashirika ya ndege yatakayotoa huduma na ongezeko la watalii na kupelekea uchumi wa nchi kukua.

Alisema, viwanja vya ndege ni kichocheo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi vinakuza na kuimarisha utalii pamoja na uhusiano wa kibiashara kati ya Zanzibar na nchi nyengine.

“Historia inaonesha kuwa sekta ya usafiri imechochea kwa kiasi kikubwa maendeleo na hapa Zanzibar kabla ya kuanza kwa usafiri wa anga, usafiri wa bahari ulitumika na kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha biashara”, alisema Dk. Shein.

Aidha alisema, ujenzi huo ulioanza katika awamu ya sita Zanzibar chini ya uongozi wa Rais mstaafu Dk. Amani Abeid Karume, ulinza kutekelezwa kwa mkopo uliotolewa na Benki ya Dunia na benki ya Exim ya China kabla ya serikali kuukamilisha kwa fedha zake.

Aidha Dk. Shein alisema ujenzi huo ulitakiwa kukamilika mwaka 2015, ila ulichelewa kwa muda wa miaka mitano kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kuchelewa kukamilika kwa mazungumzo ya nyogeza ya gharama za mradi zipatazo dola milioni 58.35 za Marekani.

“Serikali ya awamu ya saba, ilichukua jitihada za kumalizia ujenzi wa jengo hilo kama ilivyoelekezwa katika ilani ya uchaguzi mkuu wa Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020, katika ibara ya 94 kifungu cha ‘A’”, alisema Dk. Shein.

Alifafanua kuwa, kifungu hicho kinaelekeza kuwa ‘kukamilisha ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume Zanzibar ili kuongeza idadi ya abiria wanatumia kiwanja hicho, idadi ya mizigo na mapato ya serikali’.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka watendaji na watumiaji wa uwanja huo, kuwa wazalendo na kutunza miundombinu iliyowekwa ili idumu kwa kmuda mrefu.