Asema anatosha, ana sifa za uongozi

Mgombea abainisha vipaumbele 10

NA HAJI NASSOR, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema CCM haikukosea kumteua Dk. Hussein Mwinyi kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar, kwani anasifa ya uchapakazi uliotukuka, ambao wagombea wa vyama vyengine hawana.

Dk. Shein, ameeleza hayo jana katika kiwanja wa Gombani kongwe wilaya ya Chake Chake alipokuwa akizungumza na wanaCCM na wananchi kwenye uzinduzi wa kampeni kwa chama hicho na kumnadi mgombea huyo wa urais wa Zanzibar.

Alisema, CCM daima imekuwa ikiteua wagombea wa nafasi mbali mbali wenye sifa bora za kufanya kazi kwa nidhamu, uhodari na usiopendelea mtu wala kundi lolote na kuwaomba wananchi kumchagua kwa kishindo mgombea huyo.

Alieleza kuwa, Dk. Hussein Mwinyi, amekuwa akifanya kazi kwa uhodari, tokea alipokuwa katika nafasi mbali mbali za serikali na hivyo anatosha kupewa nafasi ya kuiongoza Zanzibar.

“Mpeni kura za ushindi Dk. Mwinyi, maana ni mtu bora na mchapakazi hodari na katika mazingira yoyote anafaa, maana amekuwa akipanda siku hadi siku, kwenye kuwatumikia wananchi,’’alisema.

Aidha Dk. Shein, aliwaomba wanaccm na wale wa vyama vyengine, kuhakikisha wanampigia kura za ndio mgombea huyo, ili apate ushindi ambao utaviziba mdomo vyama vyengine.

Alieleza kuwa, daima CCM imekuwa ikivuna ushindi tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini na uchaguzi wa mwanzo wa mwaka 1995, ambapo na mwaka huu 2020 kwa aina ya mgombea aliyesimamishwa kunatarajiwa ushindi mnono.

Katika hatua nyingine Dk. Shein alisema kutokana na CCM kutekeleza yale wanayoaahidi kwa wananchi kimeendelea kuwa chama bora, na imara ukilinganisha na vyama vyengine.

“Kila mmoja amekuwa akikiunga mkono chama cha Mapinduzi, kutokana na kutekeleza yale wanayoahidi mbele ya wananchi, na leo tunajivunia, ubora na uimara huo”, alisema.