NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein  jana aliongoza mazishi ya mgombea ubunge jimbo la Mpendae kupitia Chama cha Mapinduzi, Salim Hassan Abdullah Turky yaliyofanyika katika makaburi ya Kijitoupele.

Katika mazishi hayo viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa, dini, serikali, binafsi, wananchi, wafanyabiashara, ndugu na jamaa walihudhuria.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, rais mstaafu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, mzee Ali Hassan Mwinyi.

Wengine ni Makamu wa rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohamed Gharib Bilal, mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia CCM Dk. Hussein Mwinyi,  Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih na Naibu  Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali.

Awali Dk. Shein aliungana na viongozi, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi katika dua na swala ya jeneza iliyofanyika katika msikiti wa “Noor Muhammad” uliopo Mombasa.

Akisoma wasifu wa Marehemu huko Kijitoupele,  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed alisema marehemu alizaliwa Februari 11 mwaka 1963 amefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Tasakhtaa Global mjini Zanzibar.

Waziri Aboud alieleza kuwa marehemu Salim Turky alikuwa mfanyabiashara maarufu wa muda mrefu hapa nchini ambapo alianza shughuli hizo tangu miaka ya 1980 kwa kuingiza bidhaa mbali mbali.

Aliongeza kuwa katika mwaka 1990 alijiunga na kuwa mjumbe wa jumuiya ya wafanyabiashara na wakulima Zanzibar (Zanzibar National Chamber of Commence) na mwaka 2006 aliteuliwa kuwa mdhamini wa jumuiya hiyo hadi kifo chake.

Aidha, alisema kuwa katika shughuli zake za biashara marehemu alikuwa ni mwanzilishi na Mwenyekiti wa “Turky Group of Company”, kampuni ambayo inajishughulisha na bishara za utalii, mafuta na gesi, huduma za afya, viwanda, usafirishaji wa baharini na kadhalika.