NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema serikali ya awamu ya saba ilichukua jitihada za kuhakikisha inalibadilisha zao la karafuu.
Dk. Shein aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa kiwanda cha kusarifu majani makavu na yaliyoanguka wenyewe ya mkarafuu, huko Mgelema ambacho kimejengwa kwa mashirikiano ya Shirika la ZSTC na kampuni ya Indesso kutoka nchini Indonesia.
Alisema kuwa Shirika la Biashara ya Taifa (ZSTC) linakwenda kwa mabadiliko ya biashara na matumaini yake ni kwamba awamu ijayo itayaendeleza.
Aliongeza kuwa awamu ya saba iliongeza bei la zao la karafuu kutoka 3,500 hadi kufikia 14,000 huku ikisisitiza kuwa hata soko la dunia likishuka serikali itaendelea kuwalipa wakulima kwa bei hiyo.
Aliongeza kuwa uwekezaji huo ni uhusiano na ushirikiano mwema kati ya Zanzibar na Indonesia na kwamba serikali inaunga mkono kujengwa kwa kiwanda hicho kwa lengo la kufahamu kuwa Mgelema na Ngomeni ni eneo muhimu katika uzalishaji wa zao hilo.
Alisema katika kuhakikisha uimarishaji wa zao la karafuu na bidhaa zake zinaimarika, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kazi ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Alisema kuwa tayari Serikali imeshajenga barabara ya Ngomeni pamoja na kupeleka kituo cha afya, umeme na huduma nyengine hivyo, baada ya miezi miwili barabara ya kutoka Kipapo hadi Mgelema itajengwa.
Akielezea historia Dk. Shein alisema wananchi wa Zanzibar ndio waliopanda mikarafuu, lakini hawakunufaika na zao hilo na badala yake walionufaika ni watawala kabla ya mapinduzi.
Dk. Shein alieleza kuwa bado karafuu ya Zanzibar inapendwa kwani bado soko lake lipo na tayari hivi sasa karafuu imerudi hadhi yake ambapo hata magendo yamepungua.