NA RAJAB MKASABA, IKULU

SEIRIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya saba iliipa kipaumbele sekta ya  elimu ndio maana iliongeza bajeti ya Elimu na Mafunzo ya Amali kutoka shilingi bilioni 47.093 mwaka 2010/2011 hadi bilioni 178.917 mwaka 2019/2020.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alisema hayo jana katika hafla kuonana, kula chakula cha mchana pamoja na kuwakabidhi zawadi wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2019 na kidato cha sita mwaka 2019/2020 ambao wamepata ufaulu wa juu.

Dk. Shein alisema kuwa kiwango hicho cha bajeti kumeiwezesha Zanzibar kupata mafanikio makubwa katika sekta ya  elimu.

Alisema kuwa dhamira njema ya serikali, mipango mizuri tayari matunda yake yameanza kuonekana kwa kuongezeka kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya ngazi mbali mbali.

Aliongeza kuwa kwa lengo la kufikia dhamira ya kutoa elimu bure lililoongozwa na jemedari wa Mapinduzi marehemu Mzee Abeid Amani Karume Septemba 23, mwaka 1964 na awamu ya saba ilipoingia madarakani ilifanya kama zilivyofanya awamu zilizotangulia kwa kuipa kipaumbele elimu.

Alieleza kuwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao umeongezeka ambapo wanafunzi wa msingi kwenda sekondari ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 84.4 mwaka 2010 na kufikia asilimia 97.5 mwaka 2019.

Aidha alisema ufaulu wa wanafunzi kidato cha pili katika mitihani ya kuingia kidato cha tatu umeongezeka kutoka asilimia 58.2 mwaka 2010 na kufikia asilimia 76.8 mwaka 2019.

Aliongeza kuwa ufaulu wa wanafunzi kwa mitihani ya kidato cha nne kwa daraja la kwanza na pili umeongezeka mara nne zaidi kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 6.3 mwaka 2019.

Kwa upande wa kidato cha sita, alisema ufaulu kwa daraja la kwanza na la pili katika mitihani ya Taifa, kwa mwaka huu wa 2020 umefikia asilimia 33.92 ikilinganishwa na asilimia 7.2 hapo mwaka 2010.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza wanafunzi hao waliofanya vizuri wakiwemo wanafunzi 299 wa kidato cha nne na wanafunzi 124 wa kidato cha sita waliopata daraja la kwanza katika mitihani yao iliyopita.

Dk. Shein aliwapongeza kwa mafanikio hayo ambayo yameleta furaha kwao, walimu, wazazi na walezi na kuwataka waongeze bidii na  kuongeza nidhamu.

Aliwaeleza wanafunzi hao kwamba wasiwe na hofu kwani nchini vipo vyuo vikuu ambavyo vinasomesha fani mbalimbali kutokana na kuimarika kwa sekta ya elimu hapa Zanzibar.

Kwa upande wake, waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuiimarisha sekta ya elimu nchini huku akitoa pongezi nyingi kwa kutoa ufadhili wa nafasi 100 kama ni zawadi kwa kidato cha Sita waliofanya vizuri.

Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dk. Idris Muslim Hijja alieleza kuwa wanafunzi wa kidato cha nne wamefanya mtihani wa kumaliza mnamo Novemba, 2019 na matokeo kutolewa Januari 2020 ambapo jumla ya wanafunzi 18,647 walifaulu kwa madaraja mbali mbali na wanafuzi 299 wamefaulu kwa kiwango cha Daraja la Kwanza.

Aliongeza kuwa jumla ya wanafunzi 2,548 wa Kidato cha Sita walifanya mtihani wao mwezi wa Juni 2020 na matokeo yao kutoka mwezi wa Agositi 2020 wamefaulu kwa madaraja mbali mbali.

Alisema kuwa kati ya wanafunzi hao 2,548 wanafunzi 124 wamefaulu kwa kiwango cha Daraja la Kwanza ambapo katika mwaka huu wa 2020 wanafunzi bora wawili wamepatikana kwa upeo wa Tanzania kwa masomo ya Biashara.

Aliwataja kwua wanafunzi hao ni Abdulrahman Abdalla Mkanjima kwa Tahasusi ya Uchumi, Biashara na Uhasibu (ECA) kutoka Skuli ya Sekondari ya Biashara ambaye yumo katika kundi la wanafunzi 10 bora kwa Tahasusi hiyo na 10 bora kwa wanaume.

Alisema kuwa mwanafunzi mwengine ni Zaidar Bakar Hemed kwa Tahasusi ya Uchumi, Biashara na Uhasibu kutoka Skuli ya Sekondari ya Chasasa ambaye amekuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora kwa wanawake nchini Tanzania.

Wakati huo huo, Dk. Shein alitoa zawadi kwa  wanafunzi waliofanya vizuri zaidi wa kidato cha sita na kidato cha nne ambapo kwa zawadi za jumla alipata mwanafunzi Abdulrahman Abdalla Mkanjima kutoka skuli ya sekondari ya Biashara na  Ziada Bakar Hemed kutoka skuli ya Chasasa.

Kwa upande wa wanafunzi bora kidato cha nne mwaka 2019 ni Raudhat Abdalla Mselem kutoka skuli ya Fidel Castro, Khadija Hafidh Said kutoka skuli ya Lumumba na Marco Abdrea Masabuda kutoka skuli ya Mikindani.