NA HAFSA GOLO
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wasiogope kuingia ubia na wawekezaji watakaohitaji kuwekeza miradi ya maendeleo nchini ili kuendeleza maeneo yao.
Alieleza hayo jana wakati akifungua jengo la maduka ya kisasa la Sheikh Thabit Kombo linalomilikiwa kwa ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na Chama cha Mapinduzi kupitia Maskani ya Kisonge, hafla iliyofanyika uwanja wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi, Michenzani, Zanzibar.
Alisema kuingia ubia katika biashara ni moja ya hatua muhimu za mageuzi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alisema mfumo huo iwapo utatumika kwa usahihi na kufuata taratibu, utaongeza kasi ya maendeleo ya nchi na kuongeza mafanikio sambamba na kuleta maslahi endelevu katika pande zilizokubaliana.
Aidha alisema utekelezaji wa mradi huo ni moja ya hatua muhimu ya kudumisha historia pamoja na kupanua wigo na fursa nyengine mpya za kiuchumi kwa Zanzibar na wananchi wake.
Alieleza kwamba kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo na majengo mengine yaliyojengwa katika eneo la hapo kutaongeza na kupanua wigo wa ajira na wafanyabiashara kuwekeza ikilinganishwa na awali.
Hata hivyo alisema, uamuzi wa serikali kuwekeza miradi mikubwa katika eneo la Michenzani upo sahihi na unaendelea kulinda fikra na mipango ya serikali ya awamu ya kwanza iliyoongozwa na marehemu Sheikh Abeid Amani Karume kufuatia mambo mengi ya kihistoria yaliyofanyika.
Aidha Dk. Shein alisema serikali itaendelea kusimamia mipango na mikakati ya maendeleo iliyojiwekea ya kuubadilisha mji wa Zanzibar kwa kujenga nyumba za maendeleo na miradi mengine ambayo ina tija na maslahi kwa nchi.
“Mpango wetu serikali ni kuibadilisha ng’ambo ya zamani kwa kujenga nyumba za kisasa, tumeanza Kwahani, tutakuja Michenzani na eneo lote la Miembeni,” alisema.