Ni katika ujenzi wa makaazi bora, ya kisasa

NA HAFSA GOLO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amezipongeza jitihada zinazochukuliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), katika kuwekeza miradi ya maendeleo nchini ambayo inachochea kubadilisha haiba ya Zanzibar.

Dk. Shein alieleza hayo jana alipokuwa akifungua mradi wa nyumba za kisasa wa ‘ZSSF Mbweni Real Estate’ uliofanyika katika viwanja vya nyumba hizo Mbweni.

Alisema ujenzi wa mradi wa nyumba hizo za maendeleo utaleta mageuzi ya maendeleo pamoja na mji wa Mbweni kuwa wa kisasa na wenye kuwavutia wageni wanaoingia nchini.

Aidha alisema utekelezaji wa majukumu kwa ZSSF umedhihirisha matakwa ya serikali ya awamu ya saba juu ya usimamizi wa azma ya muasisi wa Mapinduzi Mzee Abeid Amani Karume katika kuhakikisha wananchi wanaishi katika makaazi bora na salama.

“ZSSF imekaza kamba na kuonesha kwa vitendo suala zima la kuimarisha miradi mbali mbali katika mji wa Zanzibar kwa kujenga miradi mikubwa ya maendeleo nchini”, alisema.

Akitilia mkazo zaidi, Dk. Shein alisema utekelezaji wa mradi huo sio jambo geni bali ni mafanikio katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020.

Aidha alisema mafanikio hayo yapo pamoja na ile azma ya malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964 katika kuhakikisha Zanzibar inaendelea kupiga hatua ya maendeleo katika makaazi bora kwa wananchi wake kwa kuzingatia mahitaji ya ardhi.

Sambamba na hilo, Dk. Shein aliwasihi wananchi walionunua nyumba hizo za maendeleo Mbweni kuzingatia sheria ili ziendelee kudumu uhalisia wake kwa kuleta haiba.

Alikemea matumizi mabaya katika nyumba hizo za kisasa badala yake aliwasihi kufuata taratibu na kuishi kwa upendo na kuheshimiana.

Dk. Shein alisema, iwapo wakaazi hao watafata tamaduni za Mzanzibari kuishi kwa upendo na kuthaminiana bila ya shaka watajenga jamii njema na yenye kuzingatia maslahi ya watu wengi katika utaratibu wao wa maisha.