DORTMUND, Ujerumani
NAHODHA wa Borussia Dortmund, Marco Reus, amefurahia mpango wa klabu hiyo wa kuendelea kufanya kazi na kiungo kutoka England, Jadon Sancho, licha ya uvumi kuwa Manchester United wanajipanga kumsajili kipindi hichi.
United walijaribu zaidi ya mara moja kuwasilisha ofa ya kumsajili kiungo huyo ili kuimarisha nguvu ya kikosi chao, lakini, walikwama kufuatia uongozi wa Dortmund kuhitaji euro milioni 120 kama ada ya usajili wa Sancho.

Sancho bado ana makataba na klabu hiyo ya Ujerumani hadi mwaka 2023 na Reus amefurahishwa kuendelea kucheza pamoja na yoso huyo wa zamani wa kikosi cha vijana cha Manchester City.

“Kwetu ni jambo kubwa, tunafuraha kwamba tutaendelea kuwa naye angalau mwaka mmoja”.
“Ndiyo kwa sababu bado anaendelea na kasi yake ya kutengeza usaidizi wa kupatikana mabao na kusumbua ngome ya upinzani, tutapata pointi nyingi”, alisema, Reus.

Hata hivyo nahodha huyo wa BVB hakuwa tayari kumfananisha Sancho na wachezaji wengine kama Lionel Messi na Christiano Ronaldo, zaidi ya kumsifia kwa kusema: “Ni mchezaji mzuri katika timu yetu na huenda siku moja atakuja kuwa mchezaji mkubwa kama wachezaji wawili (Messi na Ronaldo) tutaona.

“Anahitaji muda na uzoefu, lakini, pia kuna wakati mambo huwa hayaendi vizuri, lakini, akiwekeza bidii na kujituma atafika sababu anakipaji kikubwa.

Sancho alifunga mabao 17 msimu uliopita nyuma ya Thomas Muller (21), Timo Werner (28) na Robert Lewandowski (34) na kuwa ni mchezaji pekee aliyetoa pasi za mwisho 16 katika Ligi ya Ujerumani ya Bundesliga.(Goal)