LONDON,UINGEREZA

DUNIA inaomboleza kifo cha kiongozi wa Kuwait, Sheikh Sabah Al Ahmad Al Sabah, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91. Salamu za rambirambi zilitolewa kutoka mataifa makubwa ya Magharibi, Marekani na Uingereza, washirika wakubwa wa Kuwait, yenye utajiri wa mafuta.

Mataifa kadhaa ya Kiarabu yalitangaza siku tatu za maombolezo na kupeperusha bendera nusu mlingoti kwa heshima ya mtu anayechukuliwa kama mwanadiplomasia na mtawala wa nadra kutokuingia kwenye mitego ya kisiasa na kimadhehebu inayoligawa eneo la Ghuba.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alimuelezea Sheikh Sabah kama alama isiyo ya kawaida ya ukarimu,mjumbe wa amani,na mjengaji madaraja,baina ya pande hasimu.

Kwenye mzozo wa Qatar na mataifa mengine wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba unaoendelea hadi sasa,Sheikh Sabah alipendelea zaidi mazungumzo na anatajwa kutumia njia zake mwenyewe kujenga mawasiliano baina ya nchi hizo mbili.