ADDIS ABABA,ETHIOPIA
WAKAAZI wa Mkoa wa Tigray wa kaskazini mwa Ethiopia wanashiriki katika uchaguzi wa Bunge hatua ambayo ni kinyume kabisa na agizo la Serikali ya shirikisho ya nchi hiyo.
Hatua hiyo ilitajwa kuwa ni changamoto kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed.
Waziri Mkuu wa Ethiopia alisimamia mageuzi makubwa ya kidemokrasia tangu ashike hatamu za uongozi miaka miwili iliyopita katika nchi hiyo ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu.
Serikali ya Ethiopia na vyama vikuu vya upinzani vilikubaliana kuakhirisha uchaguzi wa taifa na wa mikoa uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi uliopita ili kudhibiti maambukizi ya corona nchini humo.
Lakini mkoa wa Tigray ambao viongozi wake wanadhibiti Serikali ya sasa wamekataa kuakhirisha uchaguzi na jana uchaguzi huo ulifanyika.
Getachew Reda,Waziri wa zamani wa habari wa Serikali ya shirikisho ya Ethiopia ambaye sasa ni msemaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray alinuukuliwa huko nyuma akisema kuwa, wanafahamu kwamba kuna vitisho vya wazi kutoka kwa Abiy Ahmed kwamba jeshi litaingilia kati na pia serikali itawakatia misaada ya fedha licha ya kuweko vitisho hivyo wao wataitisha uchaguzi kama walivyopanga.
Viongozi wa mkoa huo wanasema kuwa, kuahirishwa uchaguzi katika ngazi ya kitaifa kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19 ni kisingizio cha Waziri Mkuu Abiy Ahmed kubaki madarakani.
Kabila la Watigraya ni jamii pekee ya walio wachache nchini Ethiopia lakini ni kabila ambalo limekuwa likishikilia madaraka tangu mwaka 1991 wakati Harakati ya Kidemokrasia ya Kimapinduzi ya watu wa Ethiopia ilipomuondoa madarakani dikteta mwanajeshi mwenye mielekeo ya kimaksi, Mengistu Haile Mariam.