ADDIS ABABA,ETHIOPIA

ETHIOPIA  imetoa jibu dhaifu kwa tishio la Marekani la kuikatia misaada nchi hiyo ya Kiafrika endapo itang’ang’ania kuendelea na mradi wake katika Bwawa la al-Nahdha.

Balozi wa Ethiopia mjini Washington DC Fitsum Arega,aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijami wa Twitter kwamba,alisikia   tamko hilo la Marekani la kuzuia msaada wa dola milioni 130 kwa nchi yake na kwamba,hatua hiyo inahusiana na kadhia ya ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha.

Mwanadiplomasia huyo alisema,anasubiri maelezo zaidi hapo baadaye kutoka Serikali ya Marekani kuhusiana na uamuzi huo.

Hata hivyo balozi huyo wa Ethiopia huko Washington DC alibainisha azma iliyonayo nchi yake ya kukamilisha mradi wa ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha,ambapo aliandika katika mtandao wa Twitter kwamba wataitoa Ethiopia katika giza.

Kabla ya hapo gazeti la Foreign Policy la Marekani lilikuwa limeripoti kuwa,Serikali ya Washington imechukua uamuzi wa kusimamisha misaada yake ya nje kwa Ethiopia ikihusisha hatua hiyo na mzozo unaoshuhudiwa hivi sasa kuhusu ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha.

Mwezi uliopita Ethiopia ilinukuliwa ikitoa msimamo mkali zaidi dhidi ya Marekani ikilinganishwa na hivi  sasa.

Katika jibu dhidi ya mashinikizo ya Marekani ya kuitaka Addis Ababa isaini mkataba wa makubaliano na Misri na Sudan kuhusiana na bwawa hilo, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ethiopia Dina Mufti alisema katika kulinda maslahi yake, Ethiopia haitasalimu amri kwa mashinikizo ya Marekani na mashinikizo hayo yanaweza kupelekea kuvunjwa uhusiano wa Addis Ababa na Washington.