KIGALI,RWANDA

FAMILIA ya Paul Rusesabagina,anayezuiliwa katika jela nchini Rwanda kwa tuhuma za ugaidi inaelezea kuwa na wasiwasi wake juu ya hali yake ya afya.

Familia inaomba Rusesabagina aruhusiwe kupewa madaktari kutoka nje ya nchi ili wamuhudumie.

Rusesabagina alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza wiki moja na nusu baada ya kukamatwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, katika mazingira ya kutatanisha.

Binti yake Carine Kanimba,katika maohojiano na Sauti ya Marekani alisema kwamba baba yake alionekana ni mwenye afya dhaifu alipokuwa kizimbani.

Familia yake iliiomba Serekali ya Rwanda kumruhusu daktari kutoka nje ya nchi amchunguze hali yake ya afya na apate huduma anazohitaji.

“Tumepata taarifa kwamba hawampi dawa zake anazotumia, kuna dawa anazotakiwa kutumia kila siku. Lakini sasa tumeambiwa anapewa dawa asizozijua, na ambazo hata sisi hatuzijui. Kwa hiyo, tunaiomba Rwanda ikubali daktari wetu aje kumuhudumia.” alisema Carine.

Familia ya Rusesabagina, inaeleza pia haina imani na mawakili aliopewa Rusesabagina kutoka chama cha mawakili Rwanda, ili wamtetee katika kesi inayomkabili.

Inaomba atetewe na mawakili watakaopendekezwa na familia.

“Kusema kwamba amepewa mawakili wa kumtetea ni ujanja mtupu. Kwa sababu mawakili hao wenyewe hawakutufahamisha kama baba atafikishwa mahakamani.Huu ni ujanja kudai kuwa ana mawakili wanaomtetea, wakati hawakutupa taarifa yoyote kuhusu kufikishwa kwake mahakamani.Hii ni ishara kwamba nchini Rwanda, hakuna utawala wa sheria,”alisema binti wa Rusesabagina.