NAIROBI,KENYA

GAVANA wa Garissa Ali Korane ameshitakiwa kwa rushwa ya Shilingi milioni 233 kutoka Mpango wa Usaidizi wa Mjini Kenya uliofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Gavana huyo na wengine wanne walishtakiwa kwa kula njama ya kufanya uhalifu wa kiuchumi wa ulaghai.

Shitaka hilo alilikataa mbele ya Hakimu mkuu Douglas Ogoti. Korane pia alishitakiwa kwa kushindwa kwa makusudi kutii sheria inayohusiana na usimamizi wa fedha.

Upande wa mashitaka haupingi dhamana lakini uliitaka Mahakama  kuwapa washitakiwa masharti magumu ya dhamana.

Msaidizi wa DPP Alexander Muteti aliiomba Mahakama kumzuia gavana na washitakiwa wengine kupata ofisi zao.Muteti alisema kuzuiliwa ofisini haimaanishi kuondolewa ofisini lakini ni Gavana tu anazuiliwa kufika .

Wakili wa Korane Ahmednasir Abdullahi aliiomba Mahakama kumpa mteja wake dhamana inayofaa.

Alisema kuwa upande wa mashitaka hauwezi kutoa masharti ya kuachiliwa kwa mshitakiwa akisema Mahakama inapaswa kuzingatia dhana ya kutokuwa na hatia ya watuhumiwa.

“Hakuna uhalifu katika karatasi hii ya mashitaka ,hakuna mashitaka ambayo yanaonesha pesa zilipotea au ziliibiwa.Tutaonyesha katika kesi kwamba hakuna kosa kama inavyodaiwa na upande wa mashitaka,” alisema.

“Ni bahati mbaya kwamba hakuna ushahidi katika hatua hii ili tuweze kuonyesha Mahakama,”alisema.