ZASPOTI
Jelena Noura Hadid ‘Gigi Hadid’, ni mwanamitindo wa Marekani aliyezaliwa Aprili 23, 1995 ambae amesainiwa na Kampuni ya IMG tangu mwaka 2013.
Mnamo mwaka 2014, Hadid alijitokeza kwenye orodha ya wanamitindo 50 bora na mwaka 2016, Baraza la Mitindo ‘Britain’, lilimtaja kuwa ni mwanamitindo wa kimataifa.
Kipaji chake cha ulimbwende kilianzia akiwa na umri wa miaka miwili, baada ya kugunduliwa na Paul Marciano wa mavazi ya Guess, hivyo alianza kuwa mwanamitindo mtoto katika kampuni hiyo. Hadid ameibuka mara 35 kwenye kurasa za mbele za jarida la kimataifa la Vogue.
Mwanamitindo huyo aliyezaliwa katika jiji la Los Angles, mwenye asili ya dini ya Kiislamu, ambae baba yake ni Mpalestina Mohamed Hadid na mama yake ni Mholanzi aliyekuwa mwanamitindo wa zamani, Yalanda Hadid.
Mwanamitindo Hadid ana ndugu wa kike anayetambulika kwa jina la Bella na wa kiume Anwar, ambao wote nao ni wanamitindo, pia anao ndugu wawili wa baba mmoja, Marielle na Alana.
Mnamo mwaka 2013, Hadid alihitimu masomo yake ya sekondari, ambapo alikua nahodha wa timu ya mpira wa wavu katika timu yao ya ‘varsity’ hapo skulini, na pia alikuwa akishiriki mashindano ya kuendesha farasi.
Mwaka 2013, alihamia katika jiji la New York, ili kuendelea na masomo pamoja na taaluma yake ya uanamitindo, na kusomea saikolojia ya jinai katika ‘The New York School’, lakini aliamua kukata masomo yake na kuzingatia zaidi kazi yake ya uanamitindo.
Ndoto yake ya uanamitindo ilitimia mara tu baada kusainiwa na Kampuni ya IMG, ambako alionekana kwenye wiki ya fasheni ya jiji la New York, alipotembea kwenye onyesho la ‘Desigual’s show’.
Mnamo mwaka 2014, Hadid aliweka wazi kuwa, aligunduliwa na ugonjwa wa ‘Hashimoto’.
Pia mwaka 2016 alishambuliwa na mwanahabari Vitalii Sediuk’, na alipongezwa jinsi alivyojitetea kutoka kwake.
Mnamo mwezi Januari 2017, baada ya Donald Trump kusaini sheria ambayo ilifafanuliwa na vyombo vya habari kama ‘marufuku ya waislamu’, Hadid na dada yake, Bella waliungana na waislam wengine wa jiji la New York kupinga sheria hiyo.
Hivyo ndugu hao wakaelezewa kama “vijana wa kwanza wa Hollywood wenye nguvu na asili ya Kiislamu”
kupitia kazi yake hii ya uanamitindo, Hadid ametambulika sehemu nyingi ulimwenguni, kama mwanamitindo.
Mnamo mwaka 2015, Hadid alionekana katika kalenda ya Pirelli, na mwaka huohuo pia aliteuliwa kua balozi wa chapa ya lebo ya mavazi ya kuogelea ya Australia Seafolly.
Haikuishia hapo tu, ametokea kwenye kurasa za mbele za majarida mbali mbali maarufu kama vile, Vogue (Amerika, Paris, Italia, Uengereza, Japan, Uhispania, Australia, Italia, China), jarida la W Magazine, Elle Canada, Harper’s Bazaar (USA, Malaysia) n.k.
Pia kutokana na umahiri wake wa kutembea, amefanya kazi na kampuni nyingi za wanamitindo kama vile, Chanel, Elie Saab, Fendi, Marc Jacobs, Fenty x Puma n.k.
Hata hivyo, hakua nyuma katika masuala ya uhisani, hivyo mnamo mwaka 2018, alitangaza kuwa atafanya kazi kwa karibu na Mfuko wa Kimataifa wa Watoto (Unicef), kusaidia watoto ulimwenguni kote.
Hadid amekua kwenye uhusiano na muimbaji wa Kiingereza ‘Zayn Malik’ tangu mwishoni mwa mwaka 2015, pia alionekana kwenye nyimbo ya mpenzi wake huyo iitwayo ‘Pillow talk’.
Mnamo April 2020, Hadid alidhihirisha ujauzito wake, wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha ‘The Tonight Show’ baada ya kuanza kusambaa kwa uvumi kuhusu ujauzito huo.