NA MARYAM HASSAN

VIJIWE 14 vinavyosadikiwa ni dawa za kulevya vyenye uzito wa gramu 1.089 vimemlaza rumande mshitakiwa Anwar Ahmad Ashraka (22) mkaazi wa Fuoni Kibondeni.

Mshitakiwa huyo pia alipatina na kete 13 zenye uzito wa gramu 0.574 vyote kwa pamoja vikiwa  ni dawa za kulevya aina ya Heroin jambo ambalo ni kosa kisheria, tukio ambalo limeokea  Machi 9, mwaka jana majira ya saa 11:30 za jioni huko Jumbi Bango la Mkoa wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa huyo alipingwa kupewa dhamana na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Safia Serembe.

Pingamizi hizo alizitoa mbele ya Hakimu Saidi Hemed Khalfan wa mahakama ya mkoa Mwera ambae nae alikubaliana na upande wa mashitaka juu ya kutompa dhamana mshitakiwa huyo kwa vile kiwango alichopatikana nacho mshitakiwa hakiruhusu kupewa dhamana kwa mujibu wa sheria 7 ya mwaka 2018.

Aidha aliomba kuahirishwa kwa shauri hilo na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi kwa sababu upelelezi umekamilika.

Awali mshitakiwa baada ya kusomewa shitaka alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana, jambo ambalo lilikataliwa mahakamani hapo.