NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Green Queen’s inaendelea kugawa pointi katika michezo yake ya ligi kuu soka ya Zanzibar ya soka la wanawake baada ya juzi tena kufungwa mabao 15-0 na Women Fighter.

Mchezo huo ambao ni wa pili mfululizo kufungwa idadi hiyo ya mabao ulichezwa kwenye uwanja wa Mao Zedong B saa 10: 00 za jioni.

Katika mchezo huo miamba hiyo awali walionekana kujikaza na kujaribu kuzuia mashambulizi, lakini baadae walinzi pamoja na mlinda mlango wao walichoka na kuruhusu kuingia mabao hayo kama mvua.

Green Queen’s licha ya kufungwa mabao hayo lakini kiwango chao kimebadilika tofauti na mchezo wao wa mwanzo na New Generation.

Katika mchezo huo mabao ya Women Fighter yaliwekwa kimiyani na Dawa Haji aliyefunga mabao manne na sita yalifungwa na Asha Abdulrahman.

Mabao mengine matatu yalifungwa na Fatma Yussuf, wakati Mwanaidi Yussuf na Nasim Khalid walifunga bao moja kila mmoja.

Ligi hiyo leo itaendelea tena kwa mchezo utakaowakutanisha Green Queen’s na Jumbi Queen’s ambao utachezwa saa 10 00 za jioni uwanjani hapo.