NA ZAINAB ATUPAE
MABINGWA wa ligi daraja la pili Mkoa Mjini msimu wa mwaka 2019-2020 Gulioni FC, wameshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya kutofungana na timu ya Kombaini Mkoa wa Mjini Magharibi.
Mchezo huo wa kirafiki ulipigwa uwanja wa Mao Zedong’s ‘A’ majira ya saa 10:00 jioni, ulikuwa wa ushindani.
Hadi timu hizo zinakwenda mapumzikoni hakuna timu iliofanikiwa kuliona lango la mwenzake.
Kurudi uwanjani kumalizia kipindi cha lala salama wanaume hao waliingia na kasi kubwa huku,kila mmoja akisaka bao kwa mwenzake, lakini hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyopata bao.
Mchezo huo maalum kwa ajili ya kutolewa zawadi za kwa mabingwa hao iliyopanda daraja la kwanza kanda, ikiwemo pesa taslimu,kombe na medali,huku mchezaji bora,kipa bora walikabidhiwa zawadi viatu.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) Seif Kombo Pandu.