KINSHASA,CONGO

KATIBU  Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kutokana na ghasia na machafuko yanayoongezeka katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Antonio Guterres alisema Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa kutokana na machafuko yaliyosababisha vifo vya makumi ya raia katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri katika siku chache za hivi karibuni.

Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ilisisitiza kuwa, umoja huo unabeba jukumu la kuwalinda raia na Serikali ya Congo DR katika jitihada za kuimarisha amani na utulivu mashariki mwa nchi hiyo. 

Antonio Guterres pia alisema Umoja wa Mataifa unaunga mkono juhudi za maofisa wa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo za kuwafikisha mahakamani watu walioshambulia raia na askari wa kulinda amani wa kikosi cha umoja huo cha MONUSCO. 

Wapiganaji wa kundi la waasi la ADF kutoka Uganda wiki iliyopita walishambulia vijiji vya mkoa wa Ituri na kuua watu wasiopungua 58. 

Waziri wa Mambo ya Ndani wa DRC, Adjio Gidi alisema kuwa, idadi kubwa ya watu katika maeneo yaliyoshambuliwa walikimbia makaazi yao wakihofia usalama wa maisha yao.

Alisema ADF iliua watu 23 katika eneo la Irumu kusini mwa mkoa wa Ituri na kisha ikaua watu wengine 35 katika eneo hilo siku iliyofuatia. 

Mkaazi mmoja wa kijiji chenye misitu mikubwa cha Tshabi katika mkoa wa Ituri alinukuliwa na duru za habari akisema kuwa, wanamgambo hao walitumia bunduki, visu, mapanga na silaha nyenginezo katika mashambulio hayo.