ZASPOTI
KUFUTWA kwa michuano ya soka ya Ligi Kuu ya Muungano inatajwa kuathiri mfumo mzima wa soka la Zanzibar, kuanzia wachezaji binafsi, klabu, timu ya taifa (Zanzibar Heroes) sambamba na kupungua ushirikiano kati ya viongozi wa FAT na ZFA wakati ule.
Ingawa baadhi ya wadau hawaoni kama ni tatizo kubwa kufutwa michuano hiyo, lakini, baadhi ya wachezaji na viongozi wa zamani wanakiri kuwa wakati ule, ligi hiyo ilileta mabadiliko makubwa kisoka na baada ya kufutwa ilichukua muda Zanzibar kufanya vizuri tena nje na ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Mwandishi wa makala haya aliamua kumtafuta mchezaji na kiongozi mwandamizi wa soka, Mzee Haji Majid, ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa ZFA wilaya ya Mjini mwenye maskani yake Jang’ombe.
Majid alianza kwa kusema kuwa kwa mawazo yake binafsi mashindano hayo yalikuwa na faida nyingi, kuliko hasara ingawa hata yeye hajui vizuri ni kwa nini mashindano yalifutwa,
Pamoja na baadhi ya wadau kusema kubadilika kwa mfumo wa ligi za CECAFA na CAF au mabadiliko ya kiutawala inaweza kuwa ni miongoni mwa sababu hizo.
Mfumo ulikuwa timu tatu za juu katika ligi ya soka Zanzibar na Bara, ndizo zinakutana na kucheza nyumbani na ugenini , mshindi alikuwa anaiwakilisha Tanzania katika kombe la klabu bingwa Afrika.
Ligi hiyo ya Muungano ya soka iliwawezesha wachezaji kuwa na weledi wa soka wa aina moja Bara na Visiwani sambaba na makocha , waamuzi na viongozi kuwa karibu muda wote wa mwaka kisoka.
Pia ilisababisha timu za madaraja yote kubadilishana wachezaji kirahisi, kwa sababu wanafahamiana kimchezo ,pia wachezaji kutoka Bara walihamishiwa hapa kucheza ligi za Zanzibar.
Aliongeza kuwa hata viongozi wa (ZFA) na (FAT) wakati huo walifahamiana vizuri katika utendaji wao tofauti na siku hizi, ambao mara nyingine wanaanza kutupiana ‘madongo’ (kutofautiana).
Hata hivyo Majid alidokeza kuwa nje ya michuano Zanzibar inapata muda wa kujitangaza zaidi kimataifa, sababu kila mwaka timu zake zinacheza nje tofauti na mfumo wa kucheza Muungano, ambapo Zanzibar ilikuwa katika mwamvuli wa Tanzania na ubingwa wa Tanzania ilikuwa haichukui kila mara.
MFUMO WA LIGI YA SOKA ZANZIBAR ULIVYO KWA SASA
Majid alikumbusha kuwa kuanzi sasa mfumo wa ligi za (ZFF) umebadilika kidogo kwa sababu kulikuwa na utitiri wa timu katika baadhi ya madaraja.
Alitoa mfano wa daraja la tatu wilaya kulikuwa na timu zaidi ya 44, na ngazi ya daraja la pili wilaya kulikuwa na timu 20 hadi 25 ( kutegemea na ukubwa wa wilaya).
Aidha kiongozi Majid anabainisha kuwa mchezaji wa ligi za Zanzibar anaruhusiwa kucheza katika timu yeyote ndani ya Unguja na Pemba lakini afuate utaratibu wa ZFA katika ngazi husika.
Hata hivyo anasikitika kuwa baada ya ligi zote kumalizika wachezaji wengi visiwani huwa hawana mechi kwa muda mrefu ukitoa ile ya Kombe la Mapinduzi, ambalo huchukua timu chache, hilo linasababisha wengi wao kushuka kwa viwango vya weledi katika soka la mtu binafsi na timu zao.
Uzoefu wa Haji Majid katika uongozi tangu ujana wake na kugundua kuwa alianza kucheza ligi za wilaya ya kati ,akitokea timu ya jeshi ya kambi la Ubago ambayo baadae ilijulikana kwa jina la Scorpion mwanzoni mwa miaka ya 1980 (baada yakutoka Uganda).
Katika timu ya Ubago aliwakuta akina Bakari Sheha, Ahmed Marungu, Ali Chepe (wote marehemu), wengine ni Ali Mfaume, Omar Tojo, Ramadhan Nassor (Bure), Haji Omar, Roman Tadei, Ibrahim Ali, Abdi Juma Libowa, Mohamed Juma ambao baadhi walikuwepo katika timu hiyo tangu miaka ya 1970 chini ya Kamanda wa Kikosi Luteni mpenda michezo Kanali, Sami na Meja Mussa Sembe kwa nyakati tofauti.
Aidha, baadhi yao aliingia nao na mara moja kuanza kushiriki Michezo ya Majeshi (BAMMATA) ndipo alipoonekana kuwa ana sifa za kucheza na kuongoza.
Mwaka 1983, Haji Majid akiwa na Luteni Issa Nassor ( Kwa sasa ni Meja Jenerali Mstaafu), walihamishiwa Makao Makuu ya Jeshi Migombani ili kuanzisha tena timu ya Nyuki FC ambayo ilisamabaratika baada ya kuwa bingwa wa Zanzibar mara kadhaa katika miaka ya kati kati ya 1970.
Akiwa Nyuki SC Majid pia aliombwa akacheze katika timu ya uraiani huko Makunduchi iliyoitwa Uhuru SC na akaanza uongozi huko, wakati huo sheria za soka za Zanzibar zilikuwa zinaruhusu.
Mwaka 1984, Haji Majidi na Luteni Issa Nasoor ( Meja Jenerali Mstaafu) walikumbwa na majukumu na kulazimika kurudi katika vikosi vyao ambapo Nassor alirudi Welezo na Majid akarudi Ubago na baadaye Majid akahamishiwa Mafia mkoa wa Pwani, ambako alikuta timu ya kikosi inacheza ligi za wilaya ya Mafia.
Alicheza msimu mmoja tu na kuchaguliwa kuchezea timu ya mkoa wa Pwani na kuwalikisha timu ya mkoa huo katika la kombe la Taifa huko Bara ambako fainali zilikuwa Bagamoyo pamoja na kombe la nane nane kitaifa.
Pia Haji Majid anatajwa kuwa ni mmoja ya wachezaji ambao walijaaliwa kuna na mashuti makali, ambayo yaliwapa wakati mgumu walinda milango.
Michuano hiyo Majid alichaguliwa kuwa miongoni mwa viongozi na mchezaji bora, lakini, kwa kuhofia kuwa atakuwa upande wa Bara mara moja viongozi wa soka wa Jeshi Zanzibar.
Kanali Masoud na Mteule Nufaika ambao walikuwa katika ofisi ya michezo Migombani walimhamisha Majid wilaya ya Mafia na kumleta Migombani katika ofisi ya michezo kama kiongozi, mratibu msimamizi wa michezo wa nyuki brigedi chini ya Kapteni John Mayao.
Katika miaka ya 1987 Haji Majid wakisaidiana na kapteni Mayao walianzisha timu zaidi katika vikosi kama vile Red sea, Welezo Kids , Bavuai Rangers, Bububu SC ( ya kambi la hospitali ya jeshi), pia timu ya Migombani kids toka familia za askari Migombani.
Timu zote hizi zilishiriki ligi mbali mbali kati wilaya tofauti. Isitoshe katika miaka ya 2000 Haji Majid ndiye alifanikisha timu za madaraja tofauti wilaya ya Mjini na Magharibi kuruhusiwa kucheza ligi zao katika viwanja vya jeshi Migombani na yeye akisimamia katika taratibu za kutoka na kuingia siku zote kama mwangalizi (observer) chini ya ZFA wakati huo.
Kuanzia mwaka 1883 Pemba kulikuwa na timu ya Ukombozi FC katika Kambi la Makue ikicheza ligi za wilaya ya Wete, ambayo mara moja akina Mayao na Majid waliibadilisha jina kuitwa Kipanga FC na baadaye kuhamishiwa Unguja.
Timu hiyo ilicheza ligi kuu hadi kuchukua ubingwa wa soka Zanzibar na huko Pemba,ikaanzishwa timu ya Hardrock ambayo ipo hadi leo ikishiriki ligi.
Juhudi za Majid na Mayao ziliongeza wachezaji toka visiwani kama akina Ali Nia , Omar Nassor, Steven Kaaya hatimaye ziliiwezesha Kipanga FC kutwaa ubingwa wa Zanzibar mwaka 2001/2002 mbali na kuwa tishio katika michezo ya Majeshi.
Aidha Majid akiwa Migombani aliendelea kucheza soka la Maveterani waliokuwa kazini kama akina Ahmed Marungu , Tojo, na kutafuta wadau waliokingia katika uongozi na kuwa waamuzi kama vile akina Idd Shaban, Waziri Sheha , Manyama Bwire, Emanuel Mahimbo na wengine ambao baadhi yao walifikia kuwa waamuzi wa FIFA.
Isitoshe akiwa mratibu wa michezo alifanikiwa kuanzisha timu zaidi katika vikosi na za ligi za uraiani kama vile WelezoKids, Bavuai Rangers, Red Sea, Bubuu FC, na kule Pemba kukawa na Hardrock, ikumbukwe kuwa Majid alikuwa sekretalieti wa kudumu katika michezo ya BAMMATA na pia katika uongozi katika mashindano ya Majeshi ya Afrika Mashariki na kati.
Mzee Haji Majid alizaliwa 1953 Paje na kumaliza elimu ya msingi hapo mwaka 1967, elimu ya sekondari aliipata jeshini.
Alijiunga na Jeshi mwaka 1974 na kuhudhuria kozi za ungozi na ujuzi nje na ndani ya nchi kitu kilichomsukuma hadi kufikia cheo cha Afisa Mteule na kuwa Mkuu wa Mwandamizi wa Nidhamu katika kambi la Migombani (A/RSM) hadi alipostaafu rasmi jeshi mwaka 2005.
Mara moja alianza kujishughulisha na uongozi wa michezo uraiani ambapo kuanzia mwaka 2010 hadi 2014 akateuliwa kuwa mjumbe wa kamati tendaji . Mwaka 2011 hadi 2012 akateuliwa kuwa katibu wa ligi za central.
Mwaka 2015 akawa mjumbe wa kamati ya waamuzi na pia kamati tendaji wilaya . Mwaka 2019 akwa katibu kamati ya waamuzi mkoa wa mjini. Mwaka 2019 akachaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa ZFA wilaya ya mjini hadi leo.