NA MARYAM HASSAN

WAKILI wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Anuwar Saaduni amepinga kuondolewa kwa shitaka linalomkabili mshitakiwa Habibu Ali Habibu (23) mkaazi wa Kianga kwa sababu wamebakisha shahidi mmoja kumsikiliza.

Wakili huyo ametoa pingamizi hizo mbele ya Hakimu Hamisuu Saaduni Makanjira, ya kwamba shahidi aliyebakia ni daktari na hakuna sababu ya kuondolewa shauri hilo.

Alisema shahidi huyo walitaraji afike mahakamani lakini alishindwa kwa sababu ya kazi hivyo ameomba kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikiliza ushahidi.

Hatua ya kupinga kufutwa kwa shauri hizo zimekuja kufuatia mshitakiwa kuiomba mahakama kuliondoa shauri hilo kwa sababu ni la muda mrefu halijasikilizwa mashahidi.

Mshitakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili ikiwemo kosa la kubaka na kutorosha mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 17.

Kwa mujibu wa maelezo ya hati ya mashitaka mshitakiwa huto anadaiwa kumtorosha mtoto huyo Disemba 6 mwaka 2016 majira ya saa 4:00 za asubuhi huko Mwera Mtofaani wilaya ya Magharibi “A” mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Ilidaiwa kwamba alimtorosha mtoto huyo ambae yupo chini ya uangalizi wa wazazi wake kutoka nyumbani kwao na kumpeleka nyumbani kwa rafiki yake Kianga Chemchem, bila ya ridhaa ya wazazi wake jambo ambalo ni kosa kisheria.

Pia mshitakiwa anadaiwa kumbaka mtoto huyo majira ya saa 6:00 za mchana, bila ya ridhaa yake jambo ambalo ni kosa kisheria.

Hakimu Hamisuu, alisema kwakuwa upande wa Mashitaka umebakisha shahidi mmoja hakuna haja ya kuliondoa shauri hilo hivyo ameahirisha hadi Oktoba 7, mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza ushahidi.