NA ASIA MWALIM

HALI ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Khamis Nyange Makame maarufu Profesa Gogo (65) alieshambuliwa kwa mapanga hivi karibuni, inaendelea kuimarika akiwa anaendelea kupokea matibabu katika hospitali kuu ya Mnazimmoja, Unguja.

Muuguzi Mkunga katika hospitali hiyo anaemuhudumia mgonjwa huyo, Leluu Omar Said, alisema hali ya msanii huyo inaendelea vyema kutokana na kuwahi kupatiwa matibabu ya awali baada ya tukio hilo.

“Alipokuja kutoka Pemba alishaanza kupatiwa baadhi ya huduma, sisi tuliendeleza matibabu na hadi sasa hatujabaini tatizo jengine na jeraha lake linaendelea vizuri,” alisema.

Akizungumzia hali yake, msanii huyo pamoja na kueleza nafuu aliyoipata, alimuomba Msajili wa Vyama vya Siasa kutowafumbia macho viongozi wanaohubiri chuki na uvunjivu wa amani.

Alisema lengo la kampeni ni kila chama kutangaza sera zake na kuwaachia wananchi kufanya maamuzi.

 “Sikuweka chuki na mtu, siku moja kabla ya tukio la kujeruhiwa tulikua na mkutano wa kampeni ya kumtangaza mbunge wetu, tulifanya sherehe kubwa, tukapiga ngoma zetu kumbe watu walichukia,” alisimulia.