ZASPOTI
HALIMA Aden ni mwanamitindo wa kimarekani, amezaliwa Septemba 19, 1997, anaesifika kuwa mwanamke wa kwanza kuvaa hijabu katika mashindano ya Miss Minnesota USA, ambapo alikuwa mshindi wa nusu fainali.
Kufuatia ushiriki wake kwenye shindano hilo, Halima alipokea umakini wa kitaifa na alisainiwa kwenye kampuni ya wanamitindo ya IMG.
Halima, alisaini mkataba wa miaka mitatu na IMG, hivyo mnamo Februari 2017, alijitokeza kwa mara ya kwanza katika Wiki ya Mitindo ya New York, kwa Msimu wa 5 wa Yeezy, Baadaye aliwahi kuwa jaji wa awali na wa matangazo ya shindano la ‘Miss USA’ 2017.
Mwanamitindo huyo ambae ni wa kwanza kuvaa hijab kutembea kwenye stage za kimataifa za wanamitindo, amefanya kazi kwenye kampuni kubwa mbali mbali kama Maxmara na Millan Fashion Week.
Mnamo Juni 2017, alikua mwanamitindo wa kwanza kuvaa hijabu kwenye kurasa za mbele za jalada la Vogue Arabia, Allure, na Briteni Vogue.
Halima ambae ni Msomali aliezaliwa katika kambi ya wakimbizi ya Nairobi nchini Kenya, akiwa na umri wa miaka sita alihamia Marekani, na kuishi huko St Cloud, Minnesota.
Alisoma Shule ya Sekondari ya Apollo ambapo wanafunzi wenzake walimpigia kura kama malkia wa kurudi nyumbani, pia ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha St Cloud State.
Mnamo 2018, Aden alikua balozi wa (UNICEF) alisisitiza kuwa kazi yake inazingatia haki za watoto.
Mnamo Mei 2019, Aden alikua mwanamitindo wa kwanza kuvaa hijab na burkini katika ‘Sports Illustrated Swimsuit’
Hivyo amevunja rikodi ya kuwa mwanamitindo wa kwanza kuvaa vazi la kuogelea na hijabu.
Haikuishia hapo, kwani lengo lake ni kugeuza tasnia hiyo ili wamawale wa kiislam wafaidike kwenye suala la urembo, alisema kwenye Instagram yake kwamba kuonekana kwake katika ‘Sports Illustrate’ kunatuma ujumbe kwa jamii yake na ulimwengu kwamba “wanawake wa asili, sura, malezi tofauti, wanaweza kusimama pamoja na kusherehekewa.”
Halima alikua mwanamke wa kwanza mweusi mwenye hijab kuonyeshwa kwenye jalada la jarida la Essence, mnamo toleo la 2020 la Januari / Februari.
“Kuna wanawake wengi wa kiislamu ambao wanahisi kama hawajatimiza kiwango cha urembo katika jamii, nilitaka kuwaambia kuwa ni sawa kuwa tofauti, kwani utofauti ni mzuri pia”. alisema wakati akihojiwa na CCN.
Mwanamitindo huyo aliekuja na utofauti katika tasnia ya wanamitindo wa kimarekani, Sasa ameingia katika ulimwengu wa ubunifu wa mitindo, ameshirikiana na brand ya kawaida ya mavazi ‘Modanisa’ kutengeneza mkusanyiko wake wa kilemba na shela.
Katika mahojiano na Teen Vogue, Aden alisema kuwa vilemba vyake hivi ni kwa kila mtu, kwa wanaovaa au hata kwa wasiovaa vilemba.
Mkataba wa uanamitindo wa Halima, unajumuisha mpaka hijab yake, kwani kuvaa hijabu ameifanya kuwa ni sehemu ya kazi yake isiyoweza kujadiliwa.
MAKALA HII IMETAYARISHWA NA LAILA KEIS KUPITIA MITANDANO MBALIMBALI