NA NASRA MANZI

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Amour Hamil Bakari, amewataka wasanii kutengeneza Filamu, ambazo zinaendana na maudhui ya Zanzibar ili kusudi kuimarisha kazi zao.

Akizungumza na wasanii hao katika kuzinduzi wa  Filam ya ‘Hatiani’ iliyofanyika katika ukumbi wa Filamu Rumaisa Malindi Zanzibar.Aliwataka wasanii hao wasichoke na kuzidisha bidii kwa kutengeneza kazi nzuri.

Pia alisema wasanii ambao wameamua kutengeneza sanaa zao wenyewe, wahakikishe wanatengeneza sanaa hizo zikiwa  bora na maudhui ya Zanzibar.

Alieleza ili kutengeneza kazi nzuri kuna haja ya kujifunza kwa kuchangiana mawazo kwani, vipaji walivyokuwa navyo vya asili watakaposaidiana wana uwezo wa kuleta maudhui mapya ya Zanzibar katika sanaa zao.

“Mkitengeneza filamu zenu zikiwa bora zitaangaliwa na watu wengi na zitawapatia fursa mbali mbali, lakini endeleeni kuzichangamkia” alisema

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi binafsi ya Sanaa Mohamed Said Mwinchande alisema  lengo la filamu kusindikiza uanzishwaji wa mradi unaoitwa ‘inua kipaji kuza sanaa Zanzibar’,ambapo mradi huo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza Disemba.

“Taasisi yetu ina lengo la  kuinua na kukuza vipaji tumeiunua ili sanaa ya Zanzibar iweze kupanda kwani uwezo upo na  waigizaji wazuri tunao” alisema.