RAMALLAH,PALESTINA

HARAKATI  ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeitaka jamii ya kimataifa na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu kuchukua hatua za maana za kuokoa maisha ya mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel ambao wanakabiliwa na hatari ya maambukizi ya virusi vya corona.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Hamas, Hazim Qassem ilisema kuwa, maambukizi ya virusi vya corona vilivyowapata mateka wawili wa Kipalestina katika jela za Israel ni ishara ya uzembe wa maofisa na wasimamizi wa jela hizo.

Hazim Qassim alisema kuwa, uzembe huo ni hatari kubwa kwa maisha ya mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel na kwa msingi huo jumuiya za kimataifa zinapaswa kuchukua hatua za kuokoa maisha ya mateka hao. 

Wakati huo huo mkuu wa kitengo cha utafiti cha Kamati ya Masuala ya Mateka wa Kipalestina, Abd al-Nasser Farawanah alisema kuwa, hadi sasa mateka 20 wa Kipalestina wamepatwa na virusi vya corona katika jela za Israel. 

Farawanah alisema, utawala wa Kizayuni wa Israel haujachukua hatua yoyote ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona katika jela zake na unazuia huduma zote za matibabu kwa mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela hizo.

Karibu mateka 4,800 wa Kipalestina wanashikiliwa katika jela za utawala haramu wa Israel na 700 miongoni mwao wanasumbuliwa na magonjwa.