NA LAILA KEIS

MSHITAKIWA Seif Hamad Khamis (25), mkaazi wa kijichi Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa mjini Magharibi Unguja, amepandishwa Mahakamani kwa kosa la kuendesha chombo cha moto akiwa hakuvaa helment.

Mshitakiwa huyo alipandishwa mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe, mbele ya Hakimu Nassim Faki, ambapo Mwendesha Mashitaka koplo wa polisi Salum Ali, alidai kuwa alikamatwa na kosa la kutovaa helment wakati akiendesha chombo hicho.

Alisema kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kifungu cha 130 (1) (4) cha sheria namba 7 mwaka 2003, sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa Mahakamani hapo, Mshitakiwa huyo alilifanya kosa hilo Agosti 17, mwaka huu majira ya saa 1:00 usiku, huko Bububu polisi Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Maghatibi Unguja.

Koplo Salum, alidai kuwa Mshitakiwa huyo alikamatwa akiwa na vespa yenye nambari ya usajili Z 157 AF, akitokea upande wa Bububu skuli kuelekea kihinani.

Mshitakiwa Seif, baada ya kusomewa shitaka lake, alikubali na kuomba Mahakama imsamehe kwa kudai kuwa ndio kwanza kosa lake la kwanza.

Upande wa mashitaka, haukukubali kutoa msamaha na badala yake, ulitoa adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wote wanaoendesha vyombo vya moto bila ya kuvaa helment.

Hakimu alimpa adhabu ya kumtoza faini ya shilingi 40,000 au kwenda kutumikia katika Chuo cha Mafunzo muda wa miezi miwili.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo,ili kujinusuru kwenda kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda huo aliopangiwa.