NA MWANDISHI WETU
ZANZIBAR ni visiwa vyenye historia kubwa katika masula makuu ya maendeleo ya uchumi, siasa, kijamii na kiutamaduni.
Yote haya ni kutokana na awamu mbalimbali za uongozi tangu kule tulikotoka ambako kila ajae Zanzibar kutalii hupewa historia hii ambayo si nyengine bali ni utawala wa Kisultani.
Tunafahamu kama historia inavyoeleza kwamba wakati wa utawala wa kisultani, ambao ndio uliohodhi njia kuu zote za kiuchumi na wenyeji kuwa vibaraka.
Hapa ardhi, makaazi bora, kazi zenye tija zote ziliwanufaisha wenye kumiliki huku wakijilimbikizia mali na wenyeji ambao walifanyakazi kubwa katika mashamba ya minazi na mikarafuu waliambulia patupu.
Hatimaye baada ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoongozwa na Jemedari Hayati Abeid Amani Karume, Wazanzibari wakawa huru na Mzee wetu huyo akawa ndiye Rais wa kwanza na kuamua kwamba kila kilichopo katika kuleta tija kitawanufaisha Wazanzibari wote bila ubaguzi.
Hapo sasa mambo yakaanza kwenda sawa kutokana na hekma za Mzee Karume na wapenda amani na maendeleo waliofikiria wazo hilo.
Kulijengwa makaazi bora, elimu na matibabu yalitangazwa bure sambamba na ujenzi wa barabara.
Kufariki kwa Mzee Abeid Amani Karume hakukuwa ndio mwisho wa tija kwa Wazanzibari kwa kunufaika na mfumo wa maendeleo kwa kila Mzanzibari.
Kila awamu ya uongozi kumekuwa na uendelezaji wa malengo yale yale ya muasisi wa Uhuru wa Wazanzibar Hayati Abeid Amani Karume.
Sheikh Mwinyi Aboud Jumbe alishika usukani na kufuatiwa na wengine akiwemo Ali Hassan Mwinyi, Idris AbdulWakil, Salmin Amour, Amani Abeid Karume na hatimaye kiongozi wetu wa sasa wa awamu ya saba ambaye ni Dk. Ali Mohamed Shein.
Hakika mengi yameonekana ukilinganisha na Zanzibar ya wakati ule ni tofauti na ambayo leo hii tunaiona. Mengi yameonekana kwa dhati tunampongeza Dk. Shein kwa maendeleo aliyoyaleta. Lengo la Mapinduzi hakika limetimia.
Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) umeitekeleza ipasavyo. Kila Nyanja iliyotajwa katika Ilani ya CCM ikiwa ni azma ya kuinua uchumi wa nchi kupitia sekta mbalimbali kama Uchumi, Utamaduni, Elimu, Afya, Biashara, Viwanda, Miundombinu na mengine mengi yanaonekana kuimarika.
Dk. Shein ameweza kuuonesha umma wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kwa mafanikio aliyoyaleta Visiwani Zanzibar kwamba alistahiki kupewa ridhaa na wazanzibari waliowengi mwaka 2010 na 2015.
Kiongozi mkweli mara nyingi ni yule anaetekeleza ahadi anazozitoa wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi. Amani na utulivu ni kipimo tosha cha utendaji mzuri wa Serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Dk. Shein.
Hakuna kilicho nyuma hadi sasa kiutendaji ambacho Rais wetu amekizembea kukifanyia kazi. Sekta ya Elimu imeweza kukua kwa kuwepo mikakati imara yenye kutekelezeka. Kila anachoahidi rais hutimiza kwa vitendo na si mameno matupu.
Tumeshuhudia kuwepo kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara kila kona ya mji na vijijini.
Ustawi wa Elimu ya maandalizi hadi Chuo Kikuu ukienda sambamba na ujenzi wa majengo ya kisasa ya kujisomea yenye vifaa vinavyotosheleza ni mambo ya kujivunia.
Ujenzi wa majengo ya maduka makubwa ya kisasa (Shopping Malls) maeneo ya michenzani yatakuwa ni kichocheo kizuri cha Maendeleo ya Uchumi na Utalii Zanzibar.
Awamu ya Saba hakika imeleta mageuzi ya kiuchumi Zanzibar katika kukuza utalii wa Zanzibar ambapo idadi ya watalii imeonekana kukua kwa kasi kutokana na sera na mipango madhubuti ya Serikali.
Kama alivyoahidi Dk.Shein kuona katika uongozi wake anayaimarisha majengo ya serikali zikiwemo ofisi ili kuona kwamba azma ya maendeleo kupitia wafanyakazi wa serikalini inakua kwa kasi.
Ama hakika Wazanzibari tunapaswa kuyaenzi mazuri yote tunayoyashuhudia leo hii ili iwe historia kwa vizazi vyetu vijavyo.
Dk. Shein ni kiongozi mwenye kuona mbali na mwenye kuthamini maendeleo kwa wote, amedhihirisha ukweli kupitia ahadi zake wakati wa kampeni za uchaguzi kwa kila kipindi.
Ni imani yangu kuona kwamba katika kipindi kifupi kabla ya kumaliza muhula wake wa mwisho, ahadi zilizobakia zitatekelezwa kwa kipindi muafaka. Hongera Rais wetu Dk. Ali Mohamed Shein kwa hakika Zanzibar ya jana sio ya Leo!