NA ABOUD MAHMOUD

WASANII ni moja ya nguzo muhimu katika taifa kwani ni rahisi  kufikisha ujumbe kwa jamii husika.

Tumeshuhudia katika sehemu mbali mbali duniani wasanii hutumiwa katika kutoa elimu kwa jamii, kwa mujibu wa fani walizokuwa nazo ikiwemo uigizaji, uimbaji wa muziki mbali mbali.

Umuhimu wa wasanii hao umeweza kutatua matatizo yanayowakabili wananchi kupitia tasnia hiyo, lakini pia kuwaeleza viongozi nini kifanyike ili kupatikana yanayohitajika.

Lakini mbali na hilo umuhimu wa wasanii huonekana kwa vile ndio wanaoweza kufikisha ujumbe na kuwaelimisha wananchi  umuhimu wa mambo wanayotakiwa wayafuate.

Hivi karibuni baada ya kuzuka ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayotokana na virusi vya corona,wasanii nchini walikuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo.

Elimu waliyoitoa wasanii hao ilifanikiwa, kwani wananchi waliweza kufuhahamu nini corona na kufuata masharti waliyotakiwa kuyafuata  ya kujikinga na ugonjwa huo.

Katika kuliona hilo Tanzania ikiwa inajiandaa na uchaguzi mkuu wa viongozi kupitia nafasi mbali mbali, ikiwemo Urais, Ubunge,Uwakilishi na Udiwani.

Kutokana na hali hiyo wasanii mbali mbali nchini hususan wa muziki wamekuwa mstari wa mbele na kuwa karibu na wagombea waokwa lengo la kuwapigia kampeni.

Tumeshuhudia wasanii wa Tanzania Bara pamoja na visiwani kuandaa matamasha maalum ya kuzindua nyimbo, walizozitunga kwa ajili ya kampeni, ili kuchagua viongozi  wanaotaka kuleta maendeleo.

Matamasha hayo ya kuzindua nyimbo za kampeni yalivutia  wananchi wengi kwa kwenda kusikiliza ujumbe unaotolewa na wasanii hao.

Lakini mbali na hilo tumeona wasanii hao wakiwemo wa kizazi kipya, kwaya,taarab wakiongozana na wagombea katika sehemu mbali mbali, wakitoa burudani inayohamasisha wananchi kuwachagua viongozi hao.

Ni jambo jema kuona wasanii wa Tanzania wakionesha uzalendo wao na mapenzi kwa viongozi katika kuhakikisha lengo na madhumuni yanayokusudiwa yanafikiwa.

Wasanii wa Zanzibar nao hawajakaa nyuma katika hilo na wametoa ahadi ya kushirikiana na wagombea hao katika kila kona ya visiwa hivi kutoa burudani.

 Ni vyema kuwapongeza wasanii hao kwa kuona umuhimu wa kutoa mashirikiano ya dhati kwa wagombea, ambao wana lengo na dhamira ya kutatua shida zinazowakabili wananchi.

Mashirikiano wanayoyatoa wasanii hao ni njia muafaka na ambayo itaweza kuelimisha wananchi, kuchagua viongozi ambao wanaweza kuleta maendeleo yatakayoibadilisha Zanzibar .

Tufahamu kwamba kazi inayofanywa na wasanii hao ni kubwa sana na inahitaji kuungwa mkono,hivyo ni vyema kwa viongozi kuwaunga mkono wasanii hao, ambao walikua mstari wa mbele katika kufikisha ujumbe kwa wananchi.