RIYAD,SAUDI ARABIA
MAHAKAMA nchini Saudi Arabia imetoa hukumu katika kesi ya kuuwawa mwandishi wa gazeti la Washington Post na mkosoaji wa serikali ya Saudia Jamal Khashoggi baada ya mtoto wake wa kiume, ambaye bado anaishi katika nchi hiyo ya Kifalme, kutangaza msamaha ambao umesababisha washitakiwa watano kutotekelezewa hukumu ya kifo.
Wakati kesi hiyo inafikia mwisho nchini Saudi Arabia, kesi hiyo inaendelea kuweka kiwingu kuhusiana na nafasi ya kimataifa ya mwanamfalme mteule Mohammed bin Salman, ambaye washirika wake waliwekewa vikwazo na Marekani na Uingereza kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya kikatili, yaliyofanyika ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul.
Hukumu iliyotolewa na mahakama ya uhalifu mjini Riyadh ilitangazwa na televisheni ya taifa ya Saudi Arabia , ambayo ilitangaza maelezo machache juu ya raia nane wa nchi hiyo lakini haikuwataja majina. Mahakama hiyo iliamuru hukumu ya miaka 20 jela kwa watu watano.