NA  ARAFA MOHAMED

IDARA ya Wazee na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na (UNICEF), imewapa mafunzo ya elimu ya malezi wafanya kazi wa Ofisi ya Wilaya ya Mjini juu ya Malezi bora kwa watoto.

Mafunzo hayo ambayo yaliwakutanisha wafanya kazi wote katika Ofisi hiyo yalifanyika katika ukumbi wa Ofisi hiyo Amani Mjini Unguja.

Maafisa hao walisema kuwa, ni vyema kwa jamii ikahakikisha inawalea watoto katika malezi mazuri ambayo yatawafanya watoto kuwa na maendeleo mazuri ya hapo baadae katika maisha yao.

Mariam Khalid Kheri, Afisa Ustawi Uwezeshaji wa Wilaya ya Mjini, alisema lengo la kutoa elimu hiyo ni kuhakikisha watoto wanapata malezi bora hasa kwa watoto ambao hawana wazazi wametelekezwa.

Alisema mafunzo hayo yenye kauli mbiu ”Elimu ya maleze kwa walezi” yanatarajiwa kutolewa katika shehia mbalimbali ili kuweza kuwapata walezi watakao wasaidia katika shughuli zao za ustawi wa jamii.

Alifahamisha kuwa, Mafunzo hayo  yanatarajia kutolewa katika Mikoa mitatu ikiwemo Kaskazini Unguja, Kaskazini Pemba, na Mkoa wa Mjini Magharibi kwa Wilaya saba katika mikoa yote.

“Mafunzo haya tunatarajia kutoa katika shehia tano, tukianza na uwongozi wa Wilaya, Mikutano ya Masheha na kushuka katika shehia”alisema.

Ofisa Wanawake na Watoto alisema, wanaendelea kutoa elimu hiyo, ili kuielewesha jamii, kuhusu kuondosha ama kumaliza kabisa vitendo vya udhalilishaji hasa kwa watoto.

“Kumpiga mtoto sio kumuadabisha bali ni kumzidisha ununda, tushirikiane katika kuwalea watoto wetu ili tuweze kupunguza udhalilishaji katika jamii na kuiacha nchi kuwa na heshima”alisema.