NA MWAJUMA JUMA
JINA la timu ya New Kingi sio geni katika medali ya soka visiwani Zanzibar hasa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.Timu hii ambayo mastakimu yake yapo Kinyasini Mkoani humo, ilianzishwa mwaka 1985 kwa usajili namba ZNSC/RAC/25/1985, na sasa inashiriki ligi ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Timu hiyo ni ya wanakijiji wenyewe na ilipewa jina hilo ambapo inapatikana katika kijiji cha Kinyasini, Shehiya ya Kinyasini, Wilaya ya Kaskazini A Unguja.
Usajili wa timu hiyo ulianza msimu wa mwaka 1985-1986 na kushiriki ligi daraja la pili ngazi ya wilaya ikiwa na timu za vijana Star, Simba Mweusi, Sharp Boys, New Star, Tumaini SC, Mundu SC, Kichugamo SC na Chui, ambapo katika kipindi hicho timu zilitakiwa kupanda ligi ya mkoa ziwe mbili na timu hiyo ya New Kingi ikashika nafasi ya pili.
Nafasi ya kwanza katika ligi yao hiyo ya wilaya ilishikiliwa na timu ya New Star ya Kibeni na kuwa miongoni mwa timu zilizoshiriki ligi ya Mkoa ili kupata nafasi ya timu mbili zitakazoshiriki ligi daraja la pili taifa.
Katika msimu huo ligi ya Mkoa wa Kaskazini Unguja iliundwa na timu nne ambazo mbili kutoka wilaya ya Kaskazini A ambazo ni New King na New Star na timu mbili za wilaya ya Kaskazini B ambazo ni Aluta na Misuka.
Katika ligi hiyo timu mbili zilitakiwa kupanda daraja la kwanza Taifa na wao wakawa miongoni mwao pamoja na timu ya Misuka na timu mbili ambazo zilibakia kila moja ikarudi wilayani kwake.
Timu hiyo ilishiriki ligi daraja la kwanza Taifa katika mwaka 1989-1990 na kukutana na timu za Miembeni, Kikwajuni, Annour, JKU, African Boys, Shangani na Mafunzo, ambapo katika daraja hilo ilidumu kwa muda wa miaka 11.
Mnamo mwaka 2000 timu ya New Kingi iishuka hadi daraja la pili Taifa na 2001 ilizidi kushuka na kupelekea kucheza ligi daraja la pili wilaya ya Kaskazini A Unguja.
New Kingi licha ya kushuka daraja kwa kasi hiyo lakini haikukata tamaa na mnamo mwaka 2017, ilirudi ligi daraja la pili taifa lakini baada ya mabadiliko ya katiba ikapelekwa ligi ya Mkoa wa Kaskazini ambayo inashiriki hadi sasa.
MAFANIKIO
Timu hiyo imepata mafanikio mengi ambapo kupitia makala hii imetaja mafanikio makubwa matatu ikiwemo kuwaunganisha wana kijiji cha Kinyasini na kuwafanya kuwa wamoja, bila ya kujali itikadi zao za chama.
Kupunguza vijana kujihusisha na kujiingiza katika wimbi la mambo maovu kama vile ulevi, wizi, unyang’anyi wa kutumia silaha na mambo mengine yasiokuwa na msingi wako.
Pia wamefanikiwa kufanya mpira kama ajira kwa vijana kwani wachezaji kadhaa wamewatoa na kusajiliwa katika klabu zinazoshiriki ligi kuu ya Zanzibar.
Miongoni mwa wachezaji hao ni Ismaili Khamis Amour anaechezea Zimamoto na pia anachezea timu ya Taifa ya Zanzibar, Jaffar Khamis Rajab na Edwin Simon (Mlandege), Michael Mashoto (Mlandege) na Abasi Pili Makame (JKU).
Pia timu hiyo imepata mafanikio ya kuwa na uwanja wake mwenyewe wa kufanyia mazoezi ambao pia watarajia uwe unatumika kwa ajili ya ligi ili kuweza kujipatia mapato.
Kwa upande wa changamoto ambazo wanazo ni kutokuwa na uhakika wa kupata fedha za kuiendesha timu, ambayo mapato yake yote yanatokana na michango ya wanachama na wapenzi wao na viongozi.