YERUSALEMU,ISRAEL

SHEKHE Abdul Rahman al-Sudais, Imamu wa Msikiti mtukufu wa Makka ameshambuliwa na Waislamu katika mitandao ya kijamii kufuatia hotuba yake aliyotoa katika Sala ya Ijumaa ambayo imetafsiriwa kama hukumu ya kuhalalisha Saudi Arabia na nchi nyengine za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel.

Katika hotuba za Sala ya Ijumaa, Imamu huyo ambaye pia ni Qaarii maarufu wa Qur’ani tukufu duniani alitumia Hadithi kadhaa za Bwana Mtume Muhammad SAW pamoja na mafundisho ya mtukufu huyo kuonyesha kuwa dini ya Uislamu inahimiza na kutilia mkazo kuwaheshimu wasio Waislamu.

Shekhe Sudais aliashiria katika hotuba yake Hadithi za Bwana Mtume SAW na kuamiliana kwake kwa wema na Mayahudi, jambo ambalo limetafsiriwa na Waislamu katika maeneo mbalimbali duniani kama hatua ya kutetea na kuhalalisha harakati inayoendeshwa na baadhi ya tawala za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel.

Akinukuu Hadithi kadhaa, Shekhe  Abdul Rahman al-Sudais alisema, wakati anatawafu, Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa ameweka rehani ngao yake kwa mfanyabiashara wa Kiyahudi kwa ajili ya kupatiwa shairi na alimtendea wema jirani yake Myahudi ambaye hatimaye alimfanya asilimu.

Imamu huyo wa Masjidul-Haram alitoa kauli hiyo baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE ambayo ni mutifaki wa karibu wa Saudi Arabia kuchukua hatua iliyolaaniwa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu wa kuitambua Israel na kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na utawala huo .

Shekhe Muhammad al-Sagheer wa Misri alimkosoa vikali Shekhe Sudais akisema, alichofanya ni kufungua njia kwa Saudia ya kufanya usaliti wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.

Sheikh Muhammad al-Shinqiti wa Mauritania,alimshutumu al Sudais kwa kuitumia vibaya minbari ya Msikiti mtukufu wa Makka kushajiisha mpango wa kihaini wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.