YERUSALEMU, ISRAEL

UMOJA wa Falme za Kiarabu umetetea uamuzi wake wa kuanzisha mahusiano rasmi na Israel na kukosowa kile ulichosema ni uingiliaji kati kwa mambo ya Waarabu unaofanywa na mataifa ya kigeni, akizilenga Iran na Uturuki.

Kwenye hotuba yake mbele kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati, Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan, alidai kwamba uamuzi wa nchi yake uliotangazwa mwezi Agosti uliuzuwia mpango wa Israel kuyanyakuwa maeneo zaidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu,alinukuliwa mara kadhaa akisema mpango huo ulisitishwa kwa muda tu.

Al Nahyan aliliambia baraza hilo kwamba Imarati inatarajia kuwa Wapalestina na Waisraili watatumia fursa hiyo kurejea kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya amani ya wote na ya kudumu.

Wapalestina walizikosowa Imarati na Bahrain kwa kusaini makubaliano na Israel chini ya ushawishi wa Marekani, wakisema ni kitendo cha usaliti.