NEW YORK, Marekani
KWA mara ya tatu, rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino amekutana na rais wa Marekani, Donald Trump kujadili juu ya mustakabali wa michuano ya Kombe la Dunia tangu taifa hilo kutangazwa mwenyeji wa mwaka 2026 pamoja na nchi jirani za Mexico na Canada.
Infantino pia alihudhuria sherehe za utiaji saini ya makubaliano ya Kidiplomasia baina ya Israel, Bahrain na Umoja wa nchi za Falme za Kiarabu.


Tenda ya nchi hizo ya kuandaa fainali hizo za Kombe la Dunia ilipitishwa na wajumbe mwaka 2018 kwa kupata ushindi wa kura 134 na kuwapiku wapinzani wake, Morocco iliyopata kura 65.
Infantino na Trump pia walizungumza kuhusu kuanzisha Makao Makuu ya FIFA nchini Marekani vile vile walifanya mapitio ya ukamilifu wa maandalizi ya mashindano hayo makubwa ya soka duniani.
Marekani ilikuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1994.


Infantino pia alitembelea ofisi za utoaji haki za Marekani na kuyashukuru mashirika ya nchi hiyo kwa kazi yao nzuri ya kupingana na rushwa katika mpira wa miguu.
“Tangu nilipochaguliwa, tumeonyesha dhamira yetu ya kutokomeza vitendo vibaya ambavyo vilichafua sifa ya FIFA hapo zamani.


“Tumesisitiza nia yetu ya kushirikiana na kusaidia mamlaka katika uchunguzi wao na mashtaka ya rushwa, ambayo haina nafasi katika mpira wa miguu”.
Infantino pia alihudhuria kusainiwa kwa makubaliano ya kihistoria kati ya Bahrain, Israel na Falme za Kiarabu, ambayo yalifanywa katika Ikulu ya White House.(Goal).