BAGHDAD,IRAQ
WAZIRI wa mafuta wa Iraq Ihsan Abdul Jabbar anatarajiwa kufikia makubaliano hivi karibuni na kundi la nchi 24 zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani la OPEC+ kuhusiana na hatua ya kuongeza usafirishaji wa mafuta ghafi ya Iraq.
Waziri huyo alinukuliwa na shirika la habari la serikali INA akitowa maelezo kuhusu makubaliano hayo.
Iraq nchi ambayo ni ya pili kwa uzalishaji mkubwa wa mafuta ilishindwa katika kipindi cha nyuma kuzingatia kikamilifu masharti ya kundi hilo la OPEC ya kupunguza uzalishaji mafuta.
Hatua ambayo ilisababisha nchi hiyo kupindukia kiwango cha uzalishaji mafuta zaidi ya kilichohitaji tangu yalipotiwa saini mwaka 2016 makubaliano baina ya Opec washirika wake wakiongozwa na Urusi.
Kushuka kwa bei ya mafuta kulikotokana na hatua ya kundi la OPEC+ kupunguza uzalishaji kumeibana Iraq kiuchumi hatua ambayo imesababisha changamoto kwa serikali inayopambana kuondokana na mporomoko uliosababishwa na miaka kadhaa ya vita na ufisadi.