YERUSALEMU,ISRAEL

ISRAEL imetia saini mikataba ya kihistoria ya kurejesha uhusiano na Umoja wa Falme za Kiarabu(UAE) na Bahrain katika hatua ambayo inaweza kuleta mabadiliko makubwa ndani ya siasa za Mashariki ya Kati.

Hafla ya utiaji saini ilifanyika katika Ikulu ya Marekani kukiwa na wawakilishi kutoka nchi hizo tatu pamoja na Rais wa Marekani Donald Trump aliyekuwa mpatanishi wa makubaliano hayo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema siku hiyo ni kiini cha historia,ambapo amani itaongezeka na kujumuisha nchi nyengine za Kiarabu kumaliza kabisa mzozo wa nchi za Kiarabu na Israel.

UAE na Bahrain ni nchi za kwanza za Kiarabu kurejesha uhusiano na Israel katika kipindi cha miaka 26.

Israel imekuwa ikivutana na nchi jirani za Kiarabu kuhusiana na masuala ya Palestina tangu kuanzishwa kwake miaka zaidi ya 70 iliyopita,ila hivi karibuni, ilikubaliana na nchi hizo mbili za Kiarabu kurejesha uhusiano huo.

Makubaliano hayo yatabadili mfarakano wa muda mrefu kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu,na kuitenga Iran kwenye eneo hilo.