Matukio ya vitendo vya udhalilishaji yamekuwa yakiendelea kuripotiwa ndani ya jamii zetu licha ya juhudi kubwa zinazokuchukuliwa na Serikali pamoja na wanaharakari wanaopinga vitendo hivyo huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto.
Zipo sababu nyingi zinazoelezwa kukithiri kwa vitendo hinyo ambavyo vinawaumiza vichwa wazanzibari hadi kufikia hatua ya kuitwa janga la kitaifa lakini ninavyoamini mimi, ukosefu wa ushahidi ni miongoini mwa chanzo cha masahibu yanayoikumba jamii yetu.
Idadi kubwa ya wahanga wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia wamekuwa wakiathirika kimwili na kiakili hali ambayo inatishia kupotea kwa taifa letu la baadae na kukosa nguvukazi imara itakayosaidia kustawisha ustawi wa jamii yetu na taifa kwa ujumla .
Baadhi ya wazazi ambao watoto wao wamekumbwa na kadhia hiyo nao huamua kunyamaza kimya na kuficha uovu huo kwa kuoneana muhali hasa muhusika mkuu wa kitendo hicho anapokuwa ni mtu wa karibu na familia au mwenye dhamana fulani huku wakimuacha mtendewa akiendelea kupata madhila yasiyokuwa na hatia .
Hali imekuwa mbaya zaidi katika vituo vya polisi na mahakama baada ya kesi nyingi zinazoriotiwa kushindwa kufikia hukumu kutokana na kukosekana kwa ushahidi hali inayochangiwa na baadhi ya wananchi kutokuwa na elimu juu ya umuhimu wa kutoa ushahidi, na wengine kutokuwa tayari kutoa ushahidi kwa kuoneana muhali.
Masuala ya rushwa katika vituo vya polisi pamoja na sheria ya ushahidi kuwa na vifungu dhaifu ambavyo bado vinahitaji marekebisho nazo ni baaadhi ya changamoto zinazorejesha nyuma juhudi za mapambano ya vita vya adhalilishaji wa kijinsia.
Udhaifu huo umekuwa ukiendelea kutoa nafasi kwa wahusika wa vitenzo hivyo kuendelea kudunda mitaani bila ya hofu huku wakidhani kuwa hakuna mkono wa sheria unaoweza kuwabana na kuwachukulia hatua zinazostahiki.
Wakati Serikali ikiendelea kutafakari namna ya kukabiliana na janga la udhalilishaji Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania TAMWA kwa upande wa Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Action Aid Tanzania kupitia mradi wa kupinga vitendo vya ukatili kwa wananawake na watoto imeamua kutoa elimu inayohusiana na masuala ua ushahidi wa kisheria kwa wanachi.
Baadhi ya sheria zilizowasilishwa na wanasheria pamoja na wanaharakati katika mikutano mbalimbali ya wananchi wa mkoa wa kaskazini unguja ni sheria ya ushahidi namba 9. Ya mwaka 2016 : ambayo ni sheria kuu inayotumika katika masuala ya kutoa ushahidi katika Mahkama na polisi pale unapohitajika.
Sheria nyangine ni sheria ya mwenendo ya makosa ya jinai namba 7, ya mwaka 2018 ni sheria kuu inayotoa muongozo katika kuendesha, kuchunguza na muendelezo wa makosa ya jinai
Sheria hizo na nyenginezo iwapo wananchi watazifahamu na kuzitumia ipasavyo zitawasaidia waendesha mashtaka, Jaji au Hakimu kutoa hukumu inayostahiki na kupunguza wimbi la makosa ya udhalilishaji.
Kukataa kutoa ushahidi mahakamani unaohusiana na matukio ya udhalilishaji pia kunapelekea kutokea adhari mbalimbali za kisheria , kiuchumi na kijamii ikiwemo kuendelea kwa vitendo hivyo na kukosekana kwa haki .
Iwapo mtu atakataa kutoa ushahidi mahakamani chini ya kifungu 115 cha sheria ya makosa ya jinai kinaeleza kuwa ikiwa mshtakiwa atakataa kwenda kutoa ushahidi, mahakama itatoa amri ya kukamatwa kwa kosa la kuidharau mahakama.
Kwa mujibu wa Sheria ya ushahidi kifungu 148 (2) kinaeleza kuwa ikiwa mshtaki atatoa au kuwasilisha ushahidi wa uwongo atalazimika kufunguliwa shtaka au kutozwa faini.
Hivyo basi jamii inapaswa kuzingatia Umuhimu wa kutoa ushahidi mahakamani ili kusaidia kupatikana kwa haki ya wanaofanyiwa udhalilishaji na hivyo kupunguza vitendo hivyo ambavyo vinafanyika kinyume na silka na desturi za wazanzibari.
Watendaji wa Serikali na taasisi za kiraia zinazopigania haki za wanawake na watoto waendelee kutoa mashirikiano kwa jaamii kwa kuwapa miongozo ya masuala ya ushahidi sambamba na kuweka vituo maalum katika shehia vya kupokea taarifa za udhalilisaji.