Tanzania kama zilivyo nchi nyengine duniani, inakabiliwa na wimbi la vijana wasiokuwa na ajira.

Kutokana na mazingira hayo na hasa ikizingatiwa kuwa kundi hili ni rahisi kushawishiwa kushiriki katika matukio ya uhalifu, vijana wengi wamekuwa wakijiunga na makundi maovu na kushiriki vitendo vya utumiaji wa dawa za dawa za kulevya, unyang’anyi, udhalilishaji wa watoto na kadhalika.

Hapa dawa za kulevya ni mama wa maasi, kwani ndizo  zinazomsukuma  kijana kujiingiza katika mambo kedekede machafu, miongoni mwao ni kuzihusisha familia zao na kuziingiza katika dimbwi la ufukara.

Katika miaka ya hivi karibuni, masuala hayo yameonekana kuongezeka kwa kasi ndio maana serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama vimeanza operesheni maalum ya kuwasaka watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya.

Jinsi tatizo la dawa za kulevya lilivyokuwa kuwa nchini, baadhi ya maeneo imekuwa hatari hata kwa wananchi kupita kwani makundi ya vijana yamejiweka huko kazi ya kukaba na kupokonya.

Operesheni hiyo imezaa matunda kwani kwa mujibu wa jeshi la polisi Mkoa wa Mjini Magharibi wamewahoji vijana kadhaa washukiwa wa dawa za kulevya wakiwemo wauzaji na watumiaji.

Hizi ni hatua za kupongezwa sana kwani taratibu tunauona unga unapotea katika mji kadhaa ya Tanzania, ikiwemo Zanzibar na hata Dar es Salaam zilizokuwa vinara wa biashara hizo.

Hata hivyo, juhudi za polisi na vyombo vya dola pekee hazitoshi na kwamba kuna kila sababu kila mtu kwa nafasi yake katika jamii anapaswa kutoa ushirikiano ili ndoto ya kutokomezwa dawa za kulevya iweze kufikiwa.

Tunavyoamini wanaojishughulisha na biashara ya dawa za kulevya wako kwenye jamii tunaishi nao kwenye maisha ya kila siku, hivyo ni vyema tukahakikisha tunawafichua ili janga hili la dawa za kulevya tulimalize katika jamii yetu.

Aidha, jamii ina fursa nyengine ya kuwawezesha vijana kuishi maisha yenye manufaa kwa kuwahimiza na kuwashirikisha katika kazi za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kilimo au kubuni miradi inayoweza kuwainua kimaisha.

Miongoni mwa shughuli mashuhuri na za kiasili ambazo zimewakomboa wananchi wengi katika nchi hii ni kilimo. Vijana na watu wengine wenye umri mkubwa wanathamini kulima  kwa ajili ya biashara na chakula.

Hatua hii imewainua wengi kwani wameweza kujiendesha kimaisha wao na familia zao na pia kufanikiwa kujiepusha na makundi maovu. Dhana hiyo inaonekana sasa ambapo mahitaji  ya matumizi ya vyakula vinavyolimwa nchini kama vile mazao ya chakula, matunda na mbogamboga. 

Kosa nyengine linalofanywa na jamii ni kuwanyanyapaa hata wale waliocha matumizi ya dawa za kulevya, kufanya hivi sio busara na ni hatari kubwa kwa vijana hawa.

Kama jamii tunapaswa kuwasaidia kwa kila hali vijana wanaoacha dawa za kulevya na kuwafunza mbinu mpa ambazo zitawawezesha kujitegemea kimaisha.

Tunavyoamini ushauri na mazungumzo ya kumtia moyo ya mara kwa mara sambamba na kuweza kumpatia mtaji mdogo kijana aliyeacha dawa za kulevya kunaweza kukamuokoa kuondokana na tatizo hilo moja kwa moja.

Ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya kuimarisha ustawi wa vijana sambamba na malengo   ya kukuza uchumi na kupambana na umasikini, jamii inafaa kuchukua juhudi  kuhahakikisha vijana hawashiriki katika makundi maovu ambayo ni matokeo ya kujiingiza kwenye  uhalifu.

Ifahamike kuwa kuachiwa kwao kuendelea kufanya uhalifu kunaweza kuiweka nchi mahali pabaya kwa wananchi kukosa amani  na kushindwa kufanya kazi zao za kawaida za kujiimarisha kiuchumi.