TOKYO,JAPAN

WIZARA ya mambo ya Ndani ya Japani imesema kuwa idadi ya wazee nchini humo imeweka rikodi mpya ya juu ambapo uwiano wa wazee kwa jumla ya watu wote pia ni wa juu zaidi duniani.

Wizara hiyo iliweka wazi kwa umma takwimu hizo siku moja kabla ya nchi hiyo kuadhimisha Siku ya Heshima kwa Wazee.

Ilisema idadi ya watu wenye umri wa miaka 65 au zaidi ilifikia rikodi ya milioni 36.17 wiki iliyopita,hilo ni ongezeko la watu 300,000 kutoka mwaka uliopita.

Uwiano wa wazee kwa jumla ya watu wote nchini humo umeweka rikodi ya aslimia 28.7, likiwa ni ongezeko la alama za asilimia 0.3 kutoka mwaka uliopita.

Ongezeko hilo kwa kiasi fulani limesababishwa na idadi ya jumla ya watu nchini humo kupungua kwa 290,000.

Data za Umoja wa Mataifa pia zinaonyesha kuwa uwiano wa wazee nchini Japani ni wa juu zaidi ulimwenguni na upo juu ya Italia kwa zaidi ya alama tano za asilimia.