TOKYO, JAPAN
WAZIRI wa Japani anayesimamia maswala yanayohusiana na kundi la visiwa vinavyojulikana kama Maeneo ya Kaskazini anasema Serikali inapanga kutumia mitandao ya kijamii kuongeza uhamasishaji miongoni mwa vijana.
Urusi inadhibiti visiwa hivyo ambavyo Japani inadai kuvimiliki.Serikali inadumisha kuwa visiwa hivyo ni sehemu ya urithi wa eneo la Japani na vilikaliwa kinyume cha sheria baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Waziri wa Maswala ya Okinawa na Maeneo ya Kaskazini Kono Taro alitembelea mkoa wa kaskazini wa Hokkaido kwa mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo mapema mwezi huu.
Kutokea Rasi ya Nosappu katika mji wa Nemuro, Kono alitazama mojawapo ya visiwa hivyo ambavyo Japani inadai kuvimiliki.
Kono aliwaambia wanahabari kuwa vijana wanaendelea kuwa na ufahamu mdogo wa swala hilo na kuwa serikali inaweza kufanya mengi kuvuta nadhari yao kupitia mitandao ya kijamii.
Ziara ya kila mwaka ya bila viza visiwani humo ya wakaazi wake wa zamani ilifutwa mwaka huu kwa sababu ya mripuko wa virusi vya corona.