HATIMAYE mfalme wa Japani Naruhito ameridhia uteuzi wa mwanasiasa mashuhuri nchini humo Yoshihide Suga kuwa waziri mkuu mpya wa taifa hilo liliopo mashariki ya mbali.

Chama tawala nchini Japan cha Liberal Democratic Party (LDP), kililazimika kufanya mchakato wa kumpata waziri mkuu mpya baada ya waziri mkuu aliyepo madarakani Shinzo Abe kutangaza kujizulu.

Abe alitangaza kujiuzulu mwezi Agosti mwaka 2020 kutokana na kukabiliwa na matizo ya kiafya, ambapo kwa muda mrefu katika maisha yake amekuwa akikabiliwa na ugonjwa wa tumbo.

Baada ya mchakato wa chama kufikia uamuzi wa kumchagua Suga jina lake lililazimika kupelekwa bungeni na hivyo kupigiwa kura ya imani dhidi ya nafasi hiyo kubwa ya kiutendaji nchini humo.

Bungeni Suga alishinda kirahisi katika uchaguzi wa waziri mkuu katika bunge la Diet, ambalo ni la chini nchini Japan, baada ya kupata 314 kati ya kura zote 462 zilizopigwa.

Ushindi huo mkubwa bungeni alioupata Suga ulitarajiwa hasa ikizingatiwa kuwa

muungano unaoongozwa na chama chake cha kihafidhina, Liberal Democratic Party (LDP) kina wabunge wengi.

Kabla ya uteuzi huo, jina la Suga lilikuwa miongoni mwa majina ya wanasiasa mashahuri nchini Jpaan waliokuwa wakifikiriwa na kupewa nafasi kwamba wanaweza kuchukua nafasi ya Abe.

Suga alishindana na majina makubwa yenye haiba ya kisiasa nchini Japan waliowania nafasi hiyo kupitia mchakato wa ndani wa chama tawala nchini humo.

Mongoni mwa wanasiasa hao ni waziri wa zamani wa Ulinzi Shigeru Ishiba na Waziri wa zamani wa Mambo ya nje Fumio Kishida ambo walitangaza nia yao ya kuwania nafasi hiyo katika chama cha PLD.

Wengine ni waziri wa mambo ya nje wa sasa, Toshimitsu Motegi, naye aliwania nafasi hiyo hata hivyo waziri wa Ulinzi Taro Kono kwa upande wake aliamua  kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Waziri mkuu huyo mpya ni mshirika wa karibu wa Abe, ambapo kwa kiasi kikibwa anatarajiwa kuendeleza sera ya mtangulizi wake.

Mnamo Septemba 16 mwaka huu, Abe waziri mkuu aliyeondoka madarakani alifanya mkutano wake wa mwisho na baraza la mawaziri na kuwaambia wanahabari kwamba anajivunia utawala wake wa karibu miaka minane.

Lakini Yoshihide Suga ni nani? Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 71, ni mwana wa mkulima na mwanasiasa mkongwe anatokea katika familia ambayo maisha yake yalikuwa ya kawaida sawa na ya wajapan wengine, hali ambayo inamtofautisha na wanasiasa wengine nchini humo.

Alishika nyadhifa polepole katika ngazi ya kisiasa nchini humo, ambapo kwanza alifanya kazi kama katibu wa mbunge wa mbunge chama LDP kabla ya kuanza safari yake mwenyewe ya kisiasa, kutoka kwa uchaguzi wa baraza la manispaa hadi kuwa mwanachama wa bunge la Diet mwaka 1996.

Mnamo mwaka 2005 aliteuliwa kuwa waziri chini ya waziri mkuu wa n chi hiyo Junichiro Koizumi na baada kupata ushawishi zaidi katika baraza la mawaziri la uongozi wa Shinzo Abe.

Kama mshirika wa karibu wa Abe, alijizolea sifa kutokana na utendakazi wake na waziri mkuu anayeondoka aliunga mkono ombi lake la kuwa kiongozi wa nchi.

Wakati Mfalme Akihito alipojiuzulu mwaka 2019, Suga alipewa jukumu la kutambulisha zama mpya ya ufalme kwa Japan. Utawala wa Mfalme Naruhito utaitwa “Reiwa,” au uelewano mzuri, Suga aliliambia taifa. Na Wajapan walijibu kwa kumuita Katibu Mkuu huyo wa baraza la mawaziri “Anko Reiwa.”

Kwa sababu ameachukua hatamu ya uongozi katikati ya muhula, wachambuzi wengi wanatarajia akamilishe sehemu iliyosalia hadi uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwishoni mwa mwaka ujao.

Uchaguzi wa mwaka ujao hata hivyo, utamweka mbele ya wapiga kura wote – na mwanasisa huyo mkongwe mwenye hulka ya upole huenda akawa chaguo la kwanza la chama cha LDP, wachambuzi wanasema.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliye hudumu serikalini kwa muda mrefu anachukua uongozi katika kipindi kigumu kwa nchi hiyo ambayo uchumi wake ni wa tatu kwa ukubwa duniani

Sawa na nchi nyengine, Japan inakabiliwa na changamoto ya janga la corona ambayo imeathiri pakubwa uchumi wake ambao umedumaa kwa miaka kadhaa.

Nchi hiyo pia inakabiliwa na ongezeko la wazee katika jamii, ikisadikiwa kuwa karibu thuluthi moja ya raia wake ni wazee walio na miaka zaidi ya 65.

Suga amehudumu kwa miaka kadhaa kama mkuu wa mawaziri, wadhifa ambao ni wa pili kwa ukubwa serikalini baada ya waziri mkuu.

Tayari ameahidi kuendeleza ajenda ya utawala uliokuwepo, ikiwa ni pamoja na mpango wa mageuzi wa kiuchumi unaofahamika kama Abenomics.

“Uchaguzi wa Suga unahakikishia kuendelea kwa mipango yote mikubwa ya sera iliyozinduliwa na Shinzo,” Yuki Tatsumi, mkurugenzi wa kituo cha Stimson ambacho kinaendesha mipango ya Japan mjini Washington, alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza Suga alisema amedhamiria kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya watu wa Japani na kutimiza matarajio yao.

Suga alisema ataendeleza jitihada zilizokuwa zikifanywa na serikali ya mtangulizi wake Abe Shinzo, ambapo wananchi wengi wa Japan wana matumaini kwamba anaweza kuuhuwisha uchumi wa taifa hilo ambao umezorota kutokana na ugonjwa wa corona.