NA MWANAJUMA MMANGA

JUMUIYA ya Uhifadhi wa Mazingira ya Taifa Jozani (JECA) imesema ipo katika mchakato wa kuhamasisha zaidi wananchi suala la upandaji miti ya mikeshia kwa lengo la kutunza mazingira katika sekta ya misitu.

Naibu katibu wa jumuiya hiyo Awesu Shaban Ramadhan aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili huko Jozani wilaya ya Kati Unguja.

Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza uharibifu pamoja na upoteaji wa miti ya asili hapa Zanzibar.

Alisema imekuwa ikioteshwa miti hiyo siku hadi siku, lakini inaonekana kupungua kwa kupotea kutokana na kushamiri kwa shughuli za kijamii ikiwemo kuni, mkaa na mijenga uwa.

Alisema serikali imetenga eneo maalum la upandaji miti hiyo ili kutunza rasilimali hiyo pamoja na kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema kuwa Serikali imeona umuhimu mkubwa wa kuhifadhi misitu na ndio maana wanatoa miche ya miti mbalimbali, mashamba kwa kuwapa wananchi wake ili kutunza rasilimali hiyo.

Aidha Awasu, aliwataka wanajamii kuendelea kutunza miti sambamba na kupanda miti mingi ili kupunguza mmong’onyoko unaoweza kujitokeza.

Akizungumzia suala la wafugaji alisema, wafugaji wanaofuga wanyama kama vile ngo’mbe, mbuzi wawe makini na waangalifu juu ya wanyama wao ili kuepusha uharibifu katika miche hiyo inayopandwa.

“Wakulima wengi wamekuwa wakilalamika juu ya wafugaji kwa kufanyiwa uharibifu katika vipando vyao wanavyopanda katika mashamba jambo ambalo linawavunja moyo wakulima wengi” alisema Awesu.

Alisema wao kama kamati hawatalifumbia macho suala hilo hata mara moja na iwapo mtu amepatikana na mnyama wake hatua kali atachukuliwa dhidi yake.

Naye Mohamed Salum Haji ambae ni makamu, mwenyekiti wa jumuiya hiyo alisema kuwa wamekuwa wakipanda misitu kila baada ya kipindi cha masika katika maeneo mbalimbali ambayo yamezungukiwa na hifadhi ya taifa ya

mazingira kwa upande wa misitu na kuwapa taarifa za upandaji wa miti, hivyo wamekuwa wakichangia na kuhudhuria kwa wingi katika upandaji wa misitu hiyo.