CAIRO,MISRI
WANAHARAKATI wameanzisha kampeni katika mitandao ya kijamii ya kutaka jengo la makao makuu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yaliyoko nchini Misri ligeuzwe kuwa ukumbi wa harusi.
Hii ni baada ya Arab League kutupilia mbali rasimu ya azimio la Palestina la kulaani kitendo cha Umoja wa Falme za Kiarabu cha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel mwezi uliopita.
Mwanahakarakati wa Palestina anayeongoza kampeni hiyo, Mohammed Amas alisema tayari maelfu ya watu walitangaza kuunga mkono kampeni hiyo na kwamba wanakusudia kukusanya sahihi milioni moja ili kufanikisha mpango huo.
Alinukuliwa na shirika la habari la Middle East Eye akisema kuwa, Wakati umefika wa kulifanya jengo lenye makao makuu ya eti Arab League mjini Cairo liwe na manufaa kwa umma wote, kwa kuwa hivi sasa halifanyi kazi kwa maslahi ya mtu yoyote.
Alisema lengo la kuanzisha kampeni hiyo inayofanyika kwa njia ya intaneti ni kukosoa utendaji kazi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kwamba kampeni hiyo haina mfungamano na mrego au kundi lolote la kisiasa.
Wakati huo huo, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain, Sheikh Isa Ahmed Qassim alipinga uamuzi wa nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni akisisitiza kuwa unaenda kinyume na azma na takwa la Wabahrain.
Alisema kuna tofauti kubwa baina ya watawala na watawaliwa katika fikra, malengo na maslahi.
Serikali zilishindwa kisaikolojia, na zinataka kuwatwika wananchi mzigo huo wa kufeli,Wananchi wanapaswa kulipinga hilo.