NA LAILA KEIS

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, limefanikiwa kumkamata Ahmada Daud Mwita (26), mkaazi wa Sogea kwa kosa la wizi wa vespa, ambayo ni mali ya Bakar Omar Saleh (43) mkaazi wa Sogea.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Awadh Juma Haji, aliyasema hayo kwa waandishi wa habari wakati akitoa taarifa za matukio ya wiki yaliyotokea katika Mkoa huo, huko ofisini kwake Mwembemadema Mjini Zanzibar.

Kamanda Awadh alisema, baada ya tukio la wizi kufanyika, vespa hiyo ilifichwa kwenye nyumba inayomilikiwa na Khalifa Mussa huko Mpendae Unguja.

Alisema, inasadikika kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kuiba vespa hiyo aliamua kuificha mbali na makaazi yake, ili kuzuia watu kumuona, na muhusika kuigunduwa mali yake ilipo.

Kamanda alieleza kuwa, ilipofika Septemba 4, mwaka huu, majira ya saa 03:30 asubuhi waliweza kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na vespa hiyo maeneo ya Mpendae kwa Kificho.

Aidha alisema, upelelezi wa kesi hiyo unaendelea, na ukikamlika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.