NA ABDI SULEIMAN
MWENYEKITI wa Chama cha waandishi wa habari za mazingira Tanzania (JET) Dk. Ellen Otaru, amesema bado jamii inahitaji kupatiwa uwelewa juu ya kutumia ardhi ipasavyo, ili iishi pamoja na wanyamapori.
Alisema hayo wakati wa mafunzo ya uhifadhi, ulinzi na utalii kwa wanyamapori kwa njia ya mtandao, yaliyotolewa na JET kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), chini ya mradi unaolenga kutoa elimu ya kutokomeza ukatili na ujangili kwa wanyamapori na utalii nchini.
Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kushirikiana taasisi zote za serikali na mashirika binafsi, katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Akiwasilisha mada ya utatuzi wa migogoro inayotokana na matumizi ya ardhi, hifadhi na ufugaji na mashamba, Meneja wa machinjio ya Dodoma kutoka Wizara ya Mifugo, Victor Mwita, alisema sababu inayopeleka watu kugombania rasilimali ya ardhi hasa mali iliyopo juu ya ardhi ni kuongezeka kwa idadi ya watu na mifugo.
Alisema mifugo imeongezeka kutoka milioni 21 mwaka 1978, hadi milioni 43 mwaka 2012.
“Pamoja na kwamba nchi ni kubwa, lakini rasilimali nyingi ziko katika baadhi ya mikoa, pia kuna mambo mengine yanayopelekea kuwepo kwa ongezeko ikiwemo shughuli za kibinaadamu, kama vile madini, barabara, mabadiliko ya tabianchi na kufanya vyanzo kuwa kidogo,”alisema.