NA MWANDISHI WETU, SHINYANGA

MGOMBEA wa urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. John Pombe Magufuli, amesema anakusudia kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo kwenye awamu ya pili ya uongozi.

Dk. Magufuli alieleza hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kiwanja cha Kambarage mjini Shinyanga.

Alieleza kuwa ana dhamira ya kuifanyia makubwa Tanzania na kinachohitajika wananchi na wanachama wa CCM kumpa kura zitakazomuwezesha kushinda nafasi hiyo.

Alisema katika miaka mitano iliyopita, serikali yake imetekeleza mambo mengi ya kimaendeleo kwa wananchi na kwamba ana hofu watu wengine wakishika nafasi hiyo wanaweza kuvuruga na kurudisha nyuma hatua zilizofikiwa.

Magufuli aliwataka wabunge na madiwani mkoani humo endapo wakishinda nafasi hizo baada ya uchaguzi mkuu, wahakikishe wanawatumikia wananchi.

Alisema katika awamu ijayo Chama cha Mapinduzi, kitahakikisha majiji sita yanawekwa taa barabarani za umeme wa jua, ujenzi wa viwanja vya ndege Kigoma, Iringa, Songea, Arusha, Mtwara, Dodoma, Kahama na Shinyanga.

Akizungumzia juu ya kuinua sekta ya afya alisema katika Mkoa huo serikali imetumia shilingi bilioni 31 kwa miradi ya afya, shilingi bilioni 60.8 kwa miradi ya maji kwa vijiji 42.

Kuhusu sekta ya kilimo,  alisema yapo mambo mengi yaliyofanywa ikiwa ni pamoja na kuongeza mifugo  na chanjo, kuongeza mabwawa ya maji ya mifugo kutoka 1,384 hadi 1,842 na visima 103 hadi 225, ili kurahisisha upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo.

Alisema mradi mwengine ambao serikali inakusudia kuutekeleza ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Kisaka, Shinyanga hadi Mwanza, ambapo tayari zabuni imeshatangazwa.

Akizungumzia juu ya vyama vya ushirika, alisema vitaendelezwa kwa spidi kubwa, kwa kuhakikisha vinakuwa na uwezo wa kusimamia mifumo rasmi ya masoko ikiwemo stakabadhi ghala kwa mazao yote hususan ya kimkakati.