NA MWANDISHI WETU, ITIGI

MGOMBEA wa Urais wa Chama cha Mapinduzi, John Pombe Magufuli, amewataka Watanzania kuwanyima kura  wagombe wa upinzani wanaohubiri kutaka kuanzisha utawala wa kimajimbo wa kimakabila, jambo ambalo ni hatari kwa taifa la Tanzania.

Magufuli aliyasema hayo jana katika mkutano wake wa Kampeni uliofanyika katika Wilaya ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida katika uwanja wa Polisi Square kabla ya kuelekea mkoani Dodoma, ambapo alisema aina hiyo ya utawala umepitwa na wakati na vyema kuwakataa viongozi wanaohubiri suala hilo.

Alisema viongozi hao hawaitakii mema Tanzania, kwani wanataka kutengeza matabaka ya ukabila wakati hivi sasa wananchi wanaishi kama ndugu na wanaoana na kuishi wanapotaka.

Alisema hivi sasa kuna baadhi ya majimbo yanautajiri mkubwa wa madini, misitu mikubwa  na mbuga za wanyama, huku mengine yakiwa hayana raslimali hizo, jambo ambalo wakifuata mfumo huo wa utawala wa majimbo watabaki kuwa maskini.

Kutokana na hali hiyo, Magufuli aliwataka wananchi kukataa masuala ya utawala wa majimbo yanayotaka kuletwa, kwani wakoloni walitumia njia hiyo kutawala mataifa ya Afrika.