MAREKANI imekuwa ikichukua juhudi kubwa sana kuuaminisha ulimwengu kwamba Jamhuri ya kiislamu ya Iran ndio taifa adui mkubwa kwa walimwengu kwa wakati huu.

Tangu utawala wa Donald Trump uingie madarakani umeongeza maradufu ukali dhidi ya Iran ambapo mwaka 2018, taifa hilo lilijitoa kwenye mkataba wa kuizuia Iran kuwa na silaha za nyuklia (JCPOA) bila sababu ya msingi.

Shirika la kimataifa la nguvu za nyuklia ndilo lilipewa jukumu la kuichunguza Iran kama haikiuki mkataba huo na ripoti zote za shirika hilo kabla ya Marekani kujitoa katika mkataba huo zilizthinbitisha kuwa Iran inatekeleza vyema mkataba wa JCPOA.

Katika mkataba huo uliofikiwa mwaka 2015, Marekani ilishiriki kwenye mazungumzo na kukubaliana na kila kitu hadi siku ya mwisho ya kusainiwa, lakini mwaka 2018 ilijitoa.

Iran ilikuwa ikabiliwa na vikwazo vya kimataifa kabla ya kuafikiwa kwa mkataba wa JCPOA, ambavyo viliondolewa baada ya kukubali kusaini mkataba huo na mataifa ya Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani.

Marekani kwa sasa inafanya juhudi kubwa kuichonganisha Iran na mataifa ya kiarabu na hali ilivyo uhusiano baina ya baadhi ya mataifa ya kiarabu na Iran umedorora kwa kiasi kikubwa.

Kinyume chake mataifa ya kiarabu yanayoamini kuwa Israel ndiye adui yao mkubwa, hivi sasa yanaelezwa na Marekani kuwa taifa hilo la kiyahudi ni rafiki mkubwa.

Baada ya Marekani kujitoa katika mkataba wa JCPOA, ilitangaza kuwa itaiwekea vikwazo vikali sana Iran, vikwazo ambavyo kimsingi havionekani kuwaathiri viongozi wa taifa hilo, bali wananchi wa hali za chini ndio wataathithirika wakubwa.

Marekani inajaribu kutafuta kuungwa mkono na washirika wake hasa mataifa ya Ulaya ikiwemo Ufaransa, Uingereza na Ujerumani ili visaidie mpango wake wa kuiwekeza vikwazo Iran.

Lakini mnamo Setemba 20 mwaka huu, mataifa hayo ambayo katika migogoro mingi ya kidunia yamekuwa yakisimama nyuma ya Marekani, yametoa msimamo wa pamoja kupingwa vikwazo dhidi ya Iran kwa kile yalichoeleza kuwa uamuzi huo ni kinyume cha sheria.

Kauli kama hiyo ya kupinga vikwazo dhidi ya Iran ilitolewa pia na Urusi, hasimu mkubwa wa Marekani, ambayo ilieleza kuwa kuiwekea vikwazo Iran ni hatua na vitendo vilivyo kinyume na sheria na kimsingi haifai kutekelezwa.

Kwa mujibu wa taarifa Umoja wa Mataifa umesema hautounga mkono hatua ya kuiwekea tena Iran vikwazo kama ambavyo Marekani inataka hadi hapo atakapopewa idhini na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema umoja huo hautounga mkono hatua ya kuiwekea tena Iran vikwazo, kama ambavyo Marekani inataka hadi hapo atakapopewa idhini na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katika barua aliyomuandikia rais wa baraza hilo na kuonekana na shirika la habari la AP, Guterres amesema kuna hali ya sintofahamu iwapo waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ameanzisha mchakato au la wa kurejesha vikwazo katika azimio la Baraza la Usalama ambalo lilitia saini makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu duniani.

Waziri huyo wa Mambo ya kigeni wa Marekani, alisesema Baraza la Usalama linapaswa kuiwajibisha Iran kwa kurefusha marufuku ya silaha.

Hivi karibuni rais Donald Trump ilitangaza kuwa vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vimerejeshwa, hatua ambayo imepingwa na mataifa mengine duniani yakisema havina uhalali na vinafaa kupuuzwa.

Tangazo hilo la Marekani kwa hakika litasababisha utata wakati wa mkutano wa maofisa wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wanakutana kwa njia ya video kwa sababu ya janga la ugonjwa wa COVID-19.

Guterres alisema Baraza la Usalama halijachukua hatua yoyote baada ya kupokea barua ya Pompeo, wala hakuna mwanachama wake yeyote au rais ambaye amechukua hatua.

Katibu mkuu huyo alisema sio jukumu la katibu mkuu kuendelea na mpango huo, kana kwamba hakuna utata unaoendelea.

Kwa upande wake rais wa Iran, Hassan Rouhani amezipuuzilia mbali juhudi za Marekani kurejesha tena vikwazo kwenye nchi hiyo kwa madai kwamba Iran inakiuka makubaliano ya nyuklia.

Rais huyo alitumia fursa hiyo kuzishukuru nchi za China na Urusi ambazo zimekuwa zikiukataa mpango huo wa Marekani wa kuiwekeza vikwazo nchi yake.

“Ninazishukuru Urusi na China ambazo zimepinga kwa nguvu na kwa uthabiti, zamani na sasa, kama nchi rafiki. Pia nawashukuru wanachama wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi za Ulaya,”alisema Rouhani.

Nchi nyingine pia washirika wa Marekani wameipinga hatua hiyo. Katika barua waliyoituma siku kwa rais wa Baraza la Usalama, Uingereza, Ufaransa na Ujeurmani, nchi tatu za Umoja wa Ulaya ambazo bado zina nia thabiti ya kuendelea na makubaliano hayo, zimesema tangazo la Marekani lina athari kisheria, hivyo haiwezi kurejesha tena vikwazo kwa Iran.

Bado haijafahamika wazi hatua ambayo serikali ya Trump itachukua baada ya kupuuzwa, hasa na washirika wake wa Ulaya, ambao wameahidi kuendelea na mkataba uliopo wa nyuklia.

Kukataliwa kwa jumla kwa tangazo la Marekani, kunaweza kusababisha utawala wa Trump ambao tayari umejiondoa kwenye mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa pamoja na mikataba, kujitenga zaidi na jumuiya ya kimataifa.

Ni dhahiri kwamba iwapo pendekezo hilo litashindwa, Marekani imetishia kutengua kipengele cha mkataba wa nyuklia kinachoruhusu washirika wa mkataba huo kuutuhumu upande mwingine kwa kutotekeleza masharti ya mkataba.