Dk. Husein Mwinyi afanya kampeni za kisayansi

Ayafikia makundi yote, wasema wamkubali asilimia kwa 100

NA MWANDISHI MAALUMU PEMBA

WAKATI kampeni za siasa visiwani zikizidi kushika kasi, viongozi mbali mbali wanaendelea kuzinadi sera za vyama vyao.

Akiwa katika ufunguzi wa kampeni hapa kisiwani Pemba, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, ameleta hamasa na hisia kali kwa makundi yote yaliyohudhuria mkutano ama kusikiliza kupitia vyombo vya habari.

Dk. Hussein akiwa katika kampeni zilizoitwa jina la ‘Kampeni za kisayansi, alitembelea makundi tofauti ikiwa ni pamoja na Wawuvi, Wakulima wa mwani, wavuvi wa majongoo ya baharini, wafanyabiashara, walimu, wafanyakazi wa taasisi za Serikali, vijana wa vijiweni, Waendesha bodaboda, wanawake na makundi mengine mengi.

Yapo mengi yaliyowavutia katika ziara hiyo ya Dokta Shein ambapo pamoja na mambo mengine aliwaahidi kuwajengea mazingira mazuri makundi hayo iwapo watampa ridhaa ya kuiendesha nchi.

Kwa mfano akiwa ziara ya kuwatembelea wavuvi, Dk. Mwinyi alisema aliguswa na kero za wavuvi ambazo nyingi zao Serikali ya Awamu ya Saba ya Dokta Ali Mohamed Shein imejitajidi kuzitatua.

“Kwa kuwa muelekeo mzuri umewekwa na mtangulizi wangu naamini hayo mengine yote yatatatuka la msingi ichaguweni CCM mumaliziwe kero zenu”, alisema mgombea huyo wa urais kupitia CCM.

Aidha alisema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025, imeweka vipaumbele vinono kwa kundi la Wavuvi.

Katika ukurasa wa 200, ibara ya 149 wa Ilani hiyo inabainisha jinsi wavuvi watakavyonufaika na shughuli mbali mbali zinatakazobuniwa kama hapa inavyoeleza

“Zanzibar ina fursa maalum ya kuendeleza uchumi wake kupitia rasilimali za baharini. Katika utekelezaji wa Ilani hii, CCM itaielekeza SMZ kuimairisha uvuvi na kuongeza uzalishaji na thamani ya samaki na mazao mengine ya baharini ili kuwezesha kujitosheleza kwa mahitaji ya jamiina kupata ziada ya matumizi   ya sekta nyengine za kiuchumi na soko la nje”.

Chini ya ibara hii ya 149, vifungu vyengine kumi na vitano (15) vimewekwa ili kuchanganua utekelezaji wa ilani katika sekta ya uvuvi na rasilimali nyengine za baharini ambazo miongoni mwao Dkt Hussein Mwinyi alizifafanua.

DK. MWINYI ALIVYOKUTANA NA WAENDESHA BODABODA

Dr.Mwinyi akutana na waendesha bodaboda

Kundi jengine alilokutana nalo ni kundi la vijana waendesha bodaboda ambao wamejawa na matumaini tele katika shughuli yao hiyo.

Wakizungumza na mgombea urais huyo vijana hao walijawa na shauku kubwa kiasi kwamba walijenga matumaini makubwa iwapo Dk. Mwinyi wakimchagua.

“Tumaini letu kubwa ni kurasimishwa kwa shughuli hiyo pamoja na kuingizwa kwenye mpango wa bima ya afya, jambo ambalo Dkt Mwinyi alikubaliana nalo na kwamba Serikali atakayoiunda pindi tukimpa ridhaa na sisi vijana wa bodaboda na wananchi wengi wa Zanzibar basi atazingatia masuala hayo”, alisema mmoja wa waendesha bodaboda hao.

Mambo mengine ambayo vijana hao walimuomba Dkt Hussein Mwinyi ni pamoja na kupatiwa mikopo yenye masharti nafuu kupitia mabenki.

Na kwakuwa moja kati ya vipaumbele vilivyoainishwa kwenye ilani ya CCM ya 2025 ni kuhakikisha ajira za vijana zinaongezeka angalau vijana laki tatu (300,000) waajiriwe kwenye sekta rasmi na isiyo rasmi, kuimarishwa kwa kundi la vijana wa bodaboda ni sehemu ya utekelezaji wa ilani hiyo.

Aidha hayo pia yalijiri kwa vijana wa mkoani wakati wakimlaki mgombea Dkt Mwinyi iliongezeka baada ya kuwaahidi kama alivyowaahidi waendesha bodaboda wa Chake Chake huku nao akiwataka wajiunge kwenye umoja wao ambao itakuwa rahisi kwa Serikali kuwapatia misada.

Wakati makundi mbali mbali ya mji wa Chake Chake na vitongoji vyake wakiguswa nyoyo zao na Dkt Mwinyi, Mji wa Mkoani na vitongoji vyake uling’ara siku ya Ijumaa kuanzia majira ya saa 3 asubuhi pale Dkt Hussein Mwinyi alipokutana na vijana waendesha bodaboda katika eneo la kijiji cha Mgagadu barabara inayoelekea jimbo la Kiwani.

DK. MWINYI AKUTANA NA KUNDI LA WANAWAKE

Wanawake ni kundi muhimu sana Tanzania, umuhimu wao unapatikana kwa kuwekwa kwenye mikakati mbali mbali ya maendeleo ikiwemo kuhakikisha asilimia ya kundi la wanawake linaongezeka ama kwa Sera ni kufikia asilimia 50 kwenye vyombo vya maamuzi.

Wakati akizungumza na wanawake aliokutana nao ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo na Arki ya Mimea Wawi Chake Chake, Dokta Hussein Mwinyi alizigusa tena nyoyo za wanawake waliohudhuria mkutano huo, kwa kusema.

“Kama nilivyosema na kuahidi nikiwa Unguja, na hapa napenda kusema tena kuwa, Nitahakikisha kuwa nawapa kipaumbele wanawake kwenye serikali nitakayoiunda kwani wanawake ndio waimarishaji na wajenzi wa Chama Cha Mapinduzi”, alisema.

Kwenye ilani ya CCM imebainisha wazi namna wanawake watakavyoimarishwa kwa kupatiwa mitaji na kuhakikishiwa ustawi wao, Sura ya nane ibara ya 212 inaeleza

“ CCM inatambua uwezo mkubwa wa wanawake wa kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, hivyo Chama kitaendelea kuilekeza SMZ kuweka mkazo katika kishirikisha wanawake katika shughuli za kimaendeleo”.

Sambamba na kauli hiyo vifungu vidogo (a) hadi (d) vimeelezea hatua mbali mbali za kuchukuliwa ambazo ni kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake katika masuala ya maendeleo,kuanzisha mfuko maalum wa uwezeshaji wanawake utakaowezesha kupata mikopo ya gharama nafuu,kusimamia upatikanaji wa haki za wanawake.

Aidha Dk. Mwinyi alisema atapiga vita mila nadesturi zinazowabagua au kuwadhalilisha wanawake na kusimamia utekelezaji wa sheria na mikataba ya kimataifa inayohusu ustawi wa mwanamke na kutekeleza mkakati wa kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto. 

Kwenye Mkutano huo ambapo wanawake kutoka Pembe zote za kisiwa cha Pemba walijumuika pia kwenye kongamano la Amani, Umoja na Mshikamano wao huku mada mbali mbali zilikijadiliwa Dkt Hussein Mwinyi alisema nguvu ya wanawake katika mshikamano ni nguvu imara.

DK. MWINYI ALIVYOKUTANA NA WAFANYABIASHARA

Wafanyabiashara wa mji wa Chake Chake walipata fursa pia ya kutembelewa kwenye maeneo yao.

Mzee Salmin  na Mzee Ali Hamad ni wafanyabiashara katika mji wa Chake Chake ambao walionesha bashasha na furaha yao ya kutembelewa na mgombea huyo wa rais kwa tiketi ya CCM.

Kwakuwa biashara ni miongoni mwa nguzo kuu za uchumi wan chi yeyote ile ulimwenguni, Dkt Hussein Mwinyi aliahidi kushirikiana na wafanyabiashara hao ili kuona wanapata manufaa zaidi kwao na kwa mwananchi wa kawaida.

AKUTANA NA WANANCHI WA KAWAIDA

Dr.Mwinyi akutana na wananchi wa kawaida

Ziara ya Dkt Mwinyi kuzigusa nyoyo za wapigakura zilifikia mji wa Kiwani ambako alikutana na makundi ya wazee na vijana ambao kwao ni tunu ya pekee na kutokana na ucheshi wake kwa watu walimuahidi kumpa kura za ndiyo, ikumbukwe kuwa Jimbo la Kiwani ni miongoni mwa majimbo yenye watu wenye ukarimu na uungwana sana.

Kwa upande wa Wilaya ya Mkoani Dkt Mwinyi alifika pia kijiji cha Shamiani Kuu na Mwambe ambako mapokezi yake yalikuwa makubwa na yenye bashasha.

Huko vijana wenye hamasa na Chama Cha Mapinduzi hawakusita kumuomba mgombea huyo kuimarishiwa tawi lao la CCM jambo ambalo Mgombea alilikubali pasi na hoja hapo hapo.

Aidha Wajasiriamali wa vijiji vya Michenzani na Chokocho Wilaya ya Mkoani nao walijumuika pamoja na Dky Hussein Mwinyi siku hii ya Ijumaa, maoni yao kwa mgombea ni ukuzwaji wa shughuli za ujasiriamali na kuongeza mitaji yao.

Na kwakuwa Ilani ya CCM 2025 imeliweka wazi suala hilo, Dkt Mwinyi akawaeleza wajasiriamali hao kuwa hicho ni kipambele miongoni mwa vipambele vya CCM kwa wananchi wake.

Ziara ya Mgombea Urais wa Zanzibar kwa ChamaCha Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi kisiwani Pemba n kweli imeibua hamasa mpya kwa makundi mbali mbali ya jamii, wakiwemo wavuvi, wafanyabiashara, wazee, vijana na makundi mengine

Mwanamke wa makamu Zaituni Sheha Faki wa kijiji cha Mpene Mwambe naye hakumung’unya maneno akiwa mjasiriamali wa chakula umaarufu “mamantilie”. alisema Dkt Hussein Mwinyi ni mtu anayeonesha matumaini makubwa kwa wananchi wake.

“Mimi sijapatapo kuona hasa kiongozi mwenye huluka njema kama huyu, namkubali sana tu”, alisema Zaituni.

Wananchi wengi waliozungumza na makala haya walisema Dk Hussein Mwinyi, alisema wote kwa sasa wataelekeza nguvu zao kwa kumpa kura Dk. Mwinyi hasa kwa kuwa ameonesha nia ya kutaka kusaidia makundi yote bila ubaguzi.

Kiongozi wa waendesha bodaboda katika mji wa Chake Chake yeye aliejitambulisha kwa jina la Kassim, alisema vijana wana mwamko mkubwa katika serikali ijayo na wanamatumaini na mgombea wa CCM.

Kampeni za Dk. Mwinyi ni miongoni mwa kampeni za kisaynasi ambazo pamoja na mambo mengine lakini zinagusa makundi yote na kuwafikia wale wasio na sauti kusikilizwa moja kwa moja maoni yao.