NA MWANDISHI WETU

KWA mujibu wa Katiba zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, kila baada ya kipindi cha miaka mitano Tanzania hulazimika kufanya chaguzi mbalimbali.

Miongoni mwa chaguzi hizo ni pamoja na kumpata kiongozi wa nchi kwa maana ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yule wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Sambamba na viongozi hao wakuu wa nchi, viongozi wengine wanaochaguliwa katika kipindi hicho ni wabunge, wawakilishi kwa upande wa Zanzibar na madiwani kwa pande zote mbili.

Hivyo, uchaguzi mkuu wa kuwachagua viongozi wote unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Kwa mnasaba huo, ili mwananchi waweze kuwachagua viongozi hao ni lazima wawe wametimia miaka 18 na sehemu husika ya jimbo analoishi awe ametimiza vigezo vyote vya masharti ya ukaazi ikiwa ni pamoja na kutimia miaka mitano.

Sasa basi katika kipindi hicho mara nyingi kunatokea vishawishi mbalimbali kwa wafuasi wa vyama hususan kwa upande wa vijana ambao hutumiwa katika matukio ya uchochezi wa vurugu kwa malengo ya kufanikisha matakwa ya wale ambao wanawachagua.

Hivyo, viongozi wa vyama vya siasa na majimbo wanaotaka kura hawalazimiki kuwatumia vijana hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi huo huwagusa watu wote akinamama, watu wenye ulemavu na wazee na si kulenga kwa vijana ambao mara nyingoi ndio chanzo cha vurugu kama wanavyoonekana kwa nchi za wenzetu.

Ili kuona mambo yanakwenda kama yalivyokusudiwa si vyema kabisa kuwatumia vijana katika kuhamasisha vurugu na kuvunjika kwa amani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Pamoja na yote hayo lakini ni lazima ijuwe kama hawatakuwa na vitambulisho vya kupigia kura hawataruhusika kupiga kura.

Aidha jana Chama cha CCM tayari kimezindua kampeni zake kwa mgombea wa uraisi ilhali vyama vyengine navyo vimeshaanza kampeni zao katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Hivyo basi kwa kuwa ni nchi ya kidemokrasia wanachama wa vyama mbalimbali wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kwenda kusikiliza sera za vyama vyao ili kuona kwamba wabnawachagua viongozi wanaowapenda.

Lakini kikubwa tunachotaka kusisitiza ni kuweko kwa kampeni za amani katika uchaguzi huu na kwamba huu ni wakati mwafaka wa kuwasikiliza wagombea hasa kwa waliojiandikisha ili waweze kushiriki kuwachagua viongozi bora.

Kwa kuwa kampeni hizo tayari zimeshaanza ni vyema wagombea wa nafasi mbalimbali pamoja na wafuasi wao kutumia lugha za kistararabu ambazo hazitaleta mfarakano nchini.